• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Arsenal waikomoa Leicester

Arsenal waikomoa Leicester

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Mikel Arteta amesema kikosi chake cha Arsenal “kimeanza kuelekea anakotaka” baada ya ubabe wao kudhihirika katika ushindi wa 3-1 waliousajili dhidi ya Leicester City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Februari 28, 2021.

Arsenal walichapa Leicester uwanjani King Power siku tatu baada ya kupiga Benfica ya Ureno 3-2 jijini Turin, Italia na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Europa League kwa jumla ya mabao 4-3 msimu huu.

Matokeo hayo yaliyosajiliwa na masogora wa kocha Brendan Rodgers yaliwapotezea Leicester fursa ya kuendelea kufukuzana na Manchester City kileleni mwa jedwali la EPL.

Kichapo cha Arsenal kiliwafikia Leicester siku tatu baada ya Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech kuwaondoa kwenye mabingwa hao wa zamani wa EPL kwenye kampeni za Europa League msimu huu kwa jumla ya mabao 2-0.

Licha ya Leicester kuwekwa uongozini na Youri Tielemans katika dakika ya sita, Arsenal walisalia imara na kusawazishiwa na beki David Luiz kunako dakika ya 39 kabla ya mabao mengine kufumwa wavuni na Alexandre Lacazette na Nicolas Pepe.

Penalti iliyofungwa na Lacazette ilikuwa zao la kiungo mkabaji raia wa Nigeria, Wilfred Ndidi kuunawa mpira uliolekezwa na Pepe langoni mwa Leicester.

Kocha Mikel Arteta wa Arsenal aliwapumzisha wanasoka Bukayo Saka na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang aliyeletwa ugani kwa dakika saba za mwisho katika mechi hiyo dhidi ya Leicester ambao sasa wamepoteza jumla ya mechi sita katika uwanja wa nyumbani muhula huu.

Saka na Aubameyang walitegemewa pakubwa na Arsenal katika ushindi waliouvuna dhidi ya Benfica kwenye Europa League. Leicester kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 49, nne nyuma ya West Ham United waliopepetwa 2-1 na Man-City mnamo Februari 27. Ni pengo la pointi 13 ndilo linawatenganisha Leicester na Man-City ya kocha Pep Guardiola.

Kwa upande wao, nambari 10 Arsenal wana alama 37, mbili nyuma ya nambari nane Aston Villa waliowapiga Leeds United 1-0 mnamo Jumamosi ugani Elland Road na kuweka hai matumaini ya kusakata soka ya bara Ulaya muhula ujao.

Arsenal kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Burnley ligini kabla ya kabla ya kupimana ubabe na Tottenham Hotspur, West Ham na Liverpool kwa usanjari huo.

Kwa upande wao, Leicester walionyanyua ufalme wa EPL mnamo 2015-16, watakwaruzana na Burnley mnamo Machi 3, 2021 kabla ya kuwashukia Brighton na Sheffield United ligini kisha kupepetana na Manchester United kwenye robo-fainali za Kombe la FA.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Bingwa mara mbili wa Safari Rally Hannu Mikkola afariki

Msanii wa Rhumba awapa wakazi barakoa