• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Duale azimwa kuandaa mswada wa kuzima ngono mitandaoni

Duale azimwa kuandaa mswada wa kuzima ngono mitandaoni

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA wengi katika mitandao ya kijamii, wamemkashifu Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale kwa kupendekeza mswada utakaotoa adhabu kali kwa waenezaji wa filamu za ngono kwenye mitandao.

Hii ni kufuatia kuongezeka kwa usambazaji wa picha na filamu ngomno nchini kupitia kwa mitandao ya kijamii na tovuti nyinginezo.Endapo mswada huo utapitishwa kuwa sheria, watakaopatikana na hatia ya kusambaza picha za ngono mitandaoni watapewa adhabu ya faini ya Sh20 milioni au kifungo cha miaka 25 gerezani, au adhabu zote mbili.

Bw Duale pia amependekeza mitandao yote inayosambaza filamu chafu izimwe.Lakini jana watumizi wa mitandao ya kijamii walipuuzilia mbali pendekezo hilo, wakisema kuna mambo muhimu ambayo wabunge wanafaa kufuatilia badala ya mapendekezo hayo.

“Utazamaji ponografia au kusambaza kisiri ni kama ukahaba au ushoga.  Haya ni mambo ya kibinafsi ambayo mtu hujichagulia mwenyewe na hayahitaji kudhibitiwa na sheria. Aden Duale anafaa kujishughulisha na masuala ya ugaidi na ufisadi ambayo ni matatizo mawili makuu yanayoathiri uchumi na ustawi wetu,’ akasema wakili Donald Kipkorir.

Maoni sawa na hayo yalitolewa na maelfu ya Wakenya katika mitandao ya kijamii.Hata hivyo, viongozi wa mashirika mbalimbali na wa kidini waliunga mkono pendekezo hilo la Bw Duale.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli aliwataka wabunge na Wakenya wote kuunga mkono mswada huo akisema hatua hiyo itaendeleza na kulinda maadili na usalama wa wafanyakazi wakiwa kazini.Aliongeza kuwa mswada huo pia utalinda watoto dhidi ya dhuluma ya ngono kupitia mitandaoni.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Deliverance Mark Kariuki aliunga mkono akisema utawalinda watoto ambao huvurugwa kimaadili na picha hizo chafu.Kauli sawa ilitolewa na Mbunge wa Kiminini, Chris Wamalwa., ambaye pia ni mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge Wakatoliki.

Mswada huo ambao utawasilishwa rasmi bungeni wiki hii pia unaharamisha usambazaji wa jumbe ambazo zitafasiriwa kuwa na uwezo wa kumshawishi mtu kujihusisha na vitendo vya kigaidi.

Atakayepatikana na hatia ya kushiriki uhalifu huo atatozwa faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka mitano gerezani au adhabu zote mbili.

You can share this post!

Raila atua Pwani kufunza wakazi kusakata Reggae

Vijana walipanga kuvuruga hafla za Ruto – Polisi