• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
Raia wa Sudan ndani kwa kukaidi kulipa deni

Raia wa Sudan ndani kwa kukaidi kulipa deni

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Sudan Jumatatu aliamriwa azuiliwe korokoroni ibainike ikiwa amelipa deni la mamilioni ya pesa kabla ya kusomewa mashtaka ya kughushi stempu ya idara ya Uhamiaji.

Toni Taban Suliman Malishi hakupinga agizo la hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku azuiliwe katika kituo cha polisi cha Kilimani abaini ikiwa amelipa deni alililokuwa anadaiwa na kampuni ya Ankara.

“Uko na kesi nyingine mbele ya hii mahakama,” Bi Mutuku alimwuliza mshtakiwa.

“Ndio niko nayo,” alijibu mshtakiwa.

“Uliomba muda ulipe deni ulilokuwa unadaiwa na Ankara na hukurudi kortini kueleza ikiwa uliilipa,” hakimu alimweleza.

“Nililipa hilo deni kitambo. Wakili wangu alinieleza hakuna haja nirudi kueleza korti kwa vile nimelipa deni tayari,” Toni alijibu.

Bi Mutuku alimwamuru karani wa mahakama atafute faili hiyo nyingine kwa vile kuna kibali cha kukutia nguvuni mshtakiwa.

Mshtakiwa alielezwa kuwa atazuiliwa hadi Jumanne kisha arudishwe kortini ndipo hakimu ajifahamishe na madai hayo kwamba amelipa deni la Ankara.

“Hakuna shida.Sipingi nikirudishwa korokoroni hadi Jumanne.Wakili wangu atafika kueleza zaidi,” alisema Toni.

Kuna kibali cha kumtia nguvuni mshtakiwa.

Toni anakabiliwa na shtaka la kughushi stempu ya idara ya uhamiaji.

Pia anakabiliwa na shtaka la kupatikana akiwa humu nchini kinyume cha sheria akiwa ni raia wa Sudan.

Ameshtakiwa akishirikiana na watu wengine alijitengenezea stempu ya idara ya uhamiaji inayopigwa kwenye stakabadhi za kuwaruhusu wageni kuingia nchini.

You can share this post!

Bale angali tegemeo kubwa kambini mwa Spurs – Mourinho

Wahudumu wa tuktuk Githurai wahimizwa kushirikiana