• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Maeneo hatari kwa usalama Mathare yaorodheshwa

Maeneo hatari kwa usalama Mathare yaorodheshwa

Na SAMMY KIMATU

MATHARE

OFISA mmoja katika kaunti ya Nairobi ametaja maeneo hatari kwa usalama usiku na mchana kwa wanaotembea kwa miguu katika mtaa mmoja wa mabanda.

Naibu wa chifu katika eneo la Mabatini katika kaunti ndogo ya Mathare, Bw Njogu Mugo aliambia Taifa Leo kwamba maeneo ya Mabatini Lower ‘C’ na Mashimoni ni hatari kwa yeyote kutembea peke yako iwe ni mchana au usiku.

Maeneo yote yanapatikana katika mtaa wa mabanda wa Mathare ulioko kwenye kaunti ndogo ya Mathare.

Aidha, Bw Mugo alifafanua kwamba katika Lower 3 ‘C’ mabatini, eneo hiko ni maarufu kwa uuzaji na uvutaji bangi huku eneo la Mashimoni likijulikana kwa watu kunyang’anywa pesa na simu miongoni mwa mali nyingine.

“Kuna maeneo mawili sugu kwa uhalifu katika mtaa wa mabanda wa Mathare. Moja ni Mabatini Lower 3 ‘C’ na eneo la Mashimoni,”Bw Mugo asema.

Fauka ya hayo, Bw Mugo alisema kupitia kamati ya Nyumba Kumi inayoshirikiana na maafisa wa polisi, katika siku za hivi karibuni, wamefanikiwa kupunguza visa vya uhalifu baada ya polisi kuimarisha doria na wenyeji kujitolea kupeana habari kwa hiari.

“Tumejaribu kupunguza uhalifu siku hizi baada ya wenyeji kushirikiana na kamati ya Nyumba Kumi kuwapasha habari nao maafisa wetu wa polisi wakiimarisha doria,” Bw Mugo adokeza.

Aliwapongeza makamanda wa polisi katika kituo cha polisi cha Huruma na cha Panagani kupambana na wahalifu kwenye mtaa huo.

Mapema mwaka jana, mapambano makali yalitokea mtaani huo kufuatia msako uliofanywa na polisi kuwakamata wagemaji wa pombe haranmu ya chang’aa inayoaminika kutawala mtaa huo kwa miaka na mikaka.

“Wafanyabiashara hiyo waliwalipa vijana kuzuia polisi kukamata yeyote au kuharibu pombe ya chang’aa,’’ mdokezi wetu akasema.

Hali ya taharuki ilitanda kwa zaidi ya saa nne wakati huo huku maafisa zaidi wa kupambana na ghasia wakiongezwa siku hiyo.

Barabara ya Juja ilikuwa haipitiki huku vijana wakifunga barabara kwa mawe na kuwasha moto magurudumu ya magari.

Hatimaye, hali ya kawaida ilirudi baada ya polisi kuwashinda nguvu waandamanaji.

You can share this post!

Mswada kudhibiti mikopo ya kidijitali waandaliwa

Tunatoa huduma muhimu, tupewe chanjo ya corona, wasema...