• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wafanyabiashara Thika wapokea Sh4 milioni za Uwezo Fund

Wafanyabiashara Thika wapokea Sh4 milioni za Uwezo Fund

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika wamehimizwa kuzingatia biashara ili kujiendeleza zaidi.

Vikundi 32 vilinufaika na fedha za Uwezo Fund, mwishoni mwa wiki jana ambapo vilipokea takribani Sh4 milioni.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina aliyetoa hamasisho kwa wakazi hao, alisema biashara ndiyo njia ya pekee itakayoinua maisha yao.

Alisema Covid-19 imeathiri maisha ya watu wengi na kwa hivyo njia ya pekee ya kujikwamua ni kuanza biashara.

Alisema kila mkopo hutarajiwa kulipwa baada ya mwaka moja unusu huku wakihimizwa kuweka kitu kidogo kila siku.

“Uwezo Fund inasaidia watu waliojiunga kwa vikundi. Hiyo ndiyo njia ya pekee ya kuwapa mwelekeo wa kujiendeleza,” alisema Bw Wainaina.

Vikundi hivyo vilipokea kati ya Sh100,000 na 200,000 kulingana na miradi wanayoendeleza vijana hao.

Mbunge huyo alihimiza serikali kuongeza fedha za Uwezo ili wananchi wengi waweze kunufaika kuendesha biashara zao.

Alisema kuna kikundi cha vijana kilichopata mkopo wa Sh3 milioni na sasa wanakarabati shule za msingi kwa kupaka rangi na kuweka mzunguko wa ukuta – ua – kwenye kadhaa mjini Thika.

Mwenyekiti wa kikundi cha Purple Self Help Group cha wanachama 100, Bi Pauline Wanjiru alisema wamenufaika pakubwa kwa muda wa mwaka mmoja.

“Sisi kama kikundi tunaendesha mambo mengi kama kuwalipisha wenye haja ya kutumia turubai na viti katika hafla na mikutano tofauti. Mpango huo umetuletea faida nzuri ya kifedha,” alisema Bi Wanjiru.

Pia kuna kikundi cha vijana mjini Thika kinachoendesha uoshaji wa magari baada ya kununuliwa mtambo wa kuosha magari kupitia fedha za Uwezo.

Vijana wengi walihimizwa kujitokeza kwa wingi ili kujisajili kupokea fedha hizo badala ya kuketi bure bila kufanya lolote.

“Iwapo vijana watajikusanya kwa vikundi bila shaka watapokea fedha za Uwezo na watakuwa katika nafasi nzuri ya kujiendeleza kibiashara,” alisema Bw Wainaina.

Alisema huu ndio wakati wa vijana kujitokeza na kuonyesha ujuzi wao wa kibiashara.

You can share this post!

Osoro aachiliwa kwa dhamana

Simanzi mwanamuziki Kiambukuta akifa