• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 4:48 PM
MKU na UNITAR zaingia kwenye mkataba wa ushirikiano wa kufanya utafiti na kutoa mafunzo

MKU na UNITAR zaingia kwenye mkataba wa ushirikiano wa kufanya utafiti na kutoa mafunzo

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mafunzo na Utafiti – United Nations Institute for Training and Research (UNITAR) – zimeingia katika mkataba wa kuendesha mafunzo ya utafiti na ushirikiano na nchi nyingine katika bara la Afrika.

Ushirikiano huo unalenga maswala ya utafiti na masomo tofauti ya kozi fupi katika vyuo hivyo viwili.

Mkataba huo unalenga vyuo vya umma na vya wamiliki binafsi huku ikilenga idara ya polisi, serikali kuu na za kaunti, vyuo vya masomo na vikundi vya vijana hasa katika nchi za Africa mashariki.

Mkataba huo ulitiwa saini katika chuo cha MKU kati ya Naibu Chansela wa chuo hicho Prof Deogratious Jaganyi na naibu katibu wa UN na pia mkurugenzi katika taasisi ya UNITAR, Nikhil Seth.

MKU na UNITAR zaingia kwenye mkataba wa ushirikiano wa kufanya utafiti na kutoa mafunzo. Picha/ Lawrence Ongaro

Taasisi ya UNITAR ilibuniwa mwaka wa 1963 ili kuwapa mafunzo watu wenye umri mdogo kutoka nchi za Umoja wa mataifa ambao wana umakinifu wa mambo ambao wana ujuzi wa kuweza kusuluhisha maswala muhimu.

Kulingana na ushirikiano huo maswala mengi yatatekelezwa katika nchi za Kenya, Uganda, Randa, Sudan kusini, Burundi Nigeria, Tanzania na nchi nyinginezo katika bara la Afrika.

MKU ni miongoni mwa vyuo 1,200 kwa nchi 120 vinavyofanya kazi na UN kwa kuzingatia maswala ya amani, haki za binadamu na kushughulikia maswala ya maendeleo kwa ujumla.

Baadhi ya maswala muhimu ya masomo wanayozingatia katika mtaala wao ni kuzingatia masomo ya uzamili, na shahada za digrii kupitia mtandao wa kidijitali.

Mipango mingine ni ya kupanga mikutano ya kubadilishana mawazo ya kielimu na kuzuru sehemu tofauti ili kuelewa mengi yanayoendeshwa na wengine katika sehemu hizo.

Prof Jaganyi alisema kutafanyika masomo kuhusu amani na uongozi, maswala ya ukachero, kunyoosha misuli na michezo kwa ujumla.

Alisema kutakuwepo na masomo ya kibiashara, utamaduni, afya ya watoto, na mafunzo muhimu kuhusu magonjwa ya kuambukizana.

“Chuo chetu kinatafuta ushirikiano na wengine ili kuwapa nafasi wanafunzi kujizatiti na kujiendeleza zaidi masomoni,” alisema Prof Jaganyi.

Alisema bado wataendelea kufanya ushirikiano na vyuo na mashirika yaliyo na maono sawa na yao ili kupiga hatua zaidi kwa maswala tofauti.

Alisema watafanya juhudi kuona ya kwamba wanaweka mtaala wa elimu utakaolingana na jinsi hali vilivyo na yale mabadiliko yaliyopo kwenye masomo.

Prof Jaganyi alisema watalenga idara za polisi, jeshi, na hata walinzi wa kibinafsi na pamoja na maafisa wa serikali ili waweze kujiongezea ujuzi wa taaluma zao katika chuo chao.

“Tutajaribu kuweka kozi fupi za miezi michache ili vikundi hivyo vyote vilivyotajwa viweze kuwatuma watu wao kujiongeza elimu zaidi,” alisema Prof huyo.

Alisema chuo hicho kina maono zaidi ya kujiweka katika ramani ya ulimwengu kuhusu mwelekeo wake.

You can share this post!

Jeraha kumnyima Neymar fursa nyingine ya kucheza dhidi ya...

Bandari yafurahia uteuzi wa wachezaji wake wawili...