• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Liverpool wazamisha RB Leipzig na kujikatia tiketi ya robo-fainali za UEFA

Liverpool wazamisha RB Leipzig na kujikatia tiketi ya robo-fainali za UEFA

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL waliwapokeza RB Leipzig kutoka Ujerumani kichapo cha 2-0 mnamo Jumatano usiku katika mchuano wa mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) jijini Budapest, Hungary.

Ushindi huo uliwawezesha Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuwadengua Leipzig kwa jumla ya magoli 4-0 na kufuzu kwa robo-fainali za UEFA msimu huu.

Ni matokeo ambayo yaliweka hai matumaini ya Liverpool angalau kutia kibindoni taji hilo muhula huu baada ya kampeni zao za kuhifadhi ufalme wa EPL kudidimizwa na matokeo duni ambayo yamewashuhudia wakipoteza jumla ya mechi sita zilizopita kwa mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani wa Anfield.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, huenda Liverpool sasa wakaelekeza mawazo yao yote katika kushinda taji la UEFA msimu huu, ufanisi utakaowashuhudia wakitawazwa wafalme wa kipute hicho mara mbili chini ya kipindi cha misimu mitatu iliyopita.

Sawa na mchuano wa mkondo wa kwanza, gozi hilo la marudiano lilitandaziwa uwanjani Puskas Arena jijini Budapest kwa sababu ya ukali wa masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani.

Baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi katika kipindi cha dakika 69 za kwanza za mchezo, Liverpool hatimaye walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa fowadi matata raia wa Misri, Mohamed Salah katika dakika ya 70 kabla ya Sadio Mane kutikisa nyavu dakika nne baadaye.

Bao la Mane lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Divock Origi – mshambuliaji raia wa Ubelgiji aliye na usuli wake nchini Kenya. Wanasoka wengine waliotia fora zaidi kwa upande wa Liverpool ni kiungo Thiago Alcantara na mshambuliaji Diogo Jota aliyesajiliwa kutoka Wolves mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Liverpool watasubiri hadi Ijumaa ya Machi 19 kufahamu mpinzani wao katika hatua ya robo-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

PSG yang’oa Barcelona kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA...

Timu ya tenisi ya meza ya Kenya yaingia Qatar kwa mchujo wa...