• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MWANAMUME KAMILI: Ukipenda ama kupendwa jamani sichezee mapenzi!

MWANAMUME KAMILI: Ukipenda ama kupendwa jamani sichezee mapenzi!

Na DKT CHARLES OBENE

LEO ni leo wala hakuna cha kesho ama keshokutwa.

Mapenzi hayajandikwa kwenye kitabu cha kiada wala mtaala wa mapenzi kuasisiwa.

Mtu hawezi kusoma akaelewa muundo ama mtindo wa mapenzi. Lakini punde unapopata nafasi ya kupenda ama kupendwa jamani usichezee mapenzi.

Sijui vipi mtu anavyoweza kuchezea mapenzi, lakini nijuavyo ni kwamba wanaothubutu kuchezea mapenzi hujikuta pabaya. Kama kibe ni raha, subiri karaha! Hilo sio onyo kamwe. Ni ukweli wa mambo.

Leo inatubidi twende taratibu. Wajua nyumba ya mchwa yaitwaje? Sema! Basi sema tuendelee. Kama hujui, haidhuru! Umekwisha zaliwa wala hakuna tunachoweza kufanya kubadili hali. Mangapi butu tunayoshikilia yasitufae kitu maishani, sembushe chako kichwa? Amini usiamini! Huo mlima wanamoishi mchwa umejengwa kwa mate. Hapa tunaandika lugha yetu tuipendayo ya Kiswahili. Jamani usishawishike kutafsiri neno “mate” kwa lugha nyingine. Hii hali ya mate yanikumbusha kipenzi mama, mwanamke asiyekwisha neema. Anapenda sana kuyaweka mate kwenye konzi na kunipaka shavuni. Yeyote asiyejua maana ya ushirika hana budi kutazama kichuguu! Maadamu wawili wana kusudi moja, hakuna jambo nzuri lisilowezekana. La muhimu ni kuwepo kusudi. Leo, nataka radhi nijaribu umbea. Nikishindwa nitawaachia nyie mliokwisha zeekea jamvini wenzenu kuwatafuna kama njugu.

Mwanamume mmoja alibahatika ama niseme alijaaliwa nafasi ya kipekee akakutana na mke mwema. Kweli, mke mwema. Hata mchwa wenda waliiga bidii yake. Hajui kubebedua midomo sisemi kuiga lumbwi kubadili rangi ya macho. Aachiwe asiachiwe kitu, mwanamume atarejea nyumbani, mezani kumeandikwa vyakula vya hadhi. Mwanamke nadhifu moyoni na mwilini. Cha uhai hakifi nyayoni kwake. Cha mtu hachukii, hapokei. Kwa mtu hendi ng’o! Atafute nini kwa watu ilhali kwake ndiko kuna raha? Mumewe tayari amekwisha kumzawadia nguvu mpya. Watoto watatu ambao wamekwisha anza kwenda shule.

Kwa utulivu wake, wenye kupenda ugomvi wanakosa maana. Hata mumewe anavyopenda kunywa akalala vilabuni anatamani mtu wa kumgombeza lakini wapi! Mwanamtu anajua nafasi ya mke mwema haina kivuli. Huja mwenyewe kibubusa, ulevi umemjaa, akaingia chumbani mwingi wa shombo na kutuzi. Mwanamtu hasemi. Keshoye, ajizatiti kufua vya kufulika, kushona vilivyoraruka maana raha yake anaipata kumtunza mumewe. Tulivyo wajinga sisi wanaume tunaotunzwa vyema! Hatuna shukrani. Sisi na uso ulojaa poda ni wamoja. Tunapenda leta fedheha pasipostahili.

Mwanamume mwenye mke mwema kama huyu anatafuta nini akilewa na kulala vilabuni? Ni swali tu wala sitaki jibu. Sitaki jibu kwa maana sina hakika kwamba akili zako timamu. Sitaki kujibizana nawe. Sijafika hapo pa kujibizana na watu wanaopenda kusema bila kujua wanasema nini. Isitoshe, hata yule mke mwema hajibizani na mlevi mumewe. Nataka tuvumiliane maana amekwisha kutuonyesha kwamba mwanamke mwema haishi stahamala. Sijui mpaka hapa kama tunaelewana. Na kama hatuelewani, niwie radhi maana siwezi kukulevya.

Kama ilivyo desturi ya watu wema, nadra kutifua kivumbi ama kitibua hali. Hivi tukizungumza, mke mwema hayuko tena kwake. Amekwenda tafuta popote kichwa kukitulizia. Mlevi amempa idhini kunywa shibe yake. Lakini ulevi umemtoka mume. Kijasho kimemjaa kipajini. Machozi hayaishi kumlenga machoni. Hajui anzie wapi amalizie wapi. Sitaki kucheka maana mwanamume yuko taabani. Sisi wangwana hatuna mazoea kuwacheka wafu. Lakini nimejawa maswali lukuki akilini. Analia nini? Analilia nini? Machozi yanamlenga kwa ajili gani? Anamtafutia nini mtu ambaye hakumjali hakumheshimu? Mke kukufanya mtu wa kwako nawe huondoki vilabuni? Ameondoka ndio sasa unamwona mwema? Hawa ndio wanaume wa leo. Ndio hawa wanaume tunaofukuzana nao kila siku.

Wanaume sampuli hii ndio kwanza wanazidi zaliwa. Yaani watu wanaobeba vya kubebeka waonekane kwamba ni wanaume lakini akili zao zilikwisha hama. Mtu hutafuta kitu chema akakihifadhi kimfaidi daima. Mwanamume humtafuta mwanamke mwema kumfaa daima. Lakini nyie mnaotafuta wanawake wema na kuwaweka nyumbani huku mnapapasana usiku kucha na magogo kwenye mabaa ni watu wa aina gani?

Hebu niwaelezeni nyie wenye hizi tabia za kuudhi. Dunia iko mbioni kusawazisha hali. Huku gumegume wakizidi zaliwa bila akili wanawake wema ndio kwanza wanazidi kuondoka duniani na nafasi zao kuchukuliwa na sampuli nyingine. Hali hii itaendelea hadi pale ambapo walevi wanapatana na walevi wenzao. Hapo ndipo mwanamume kamili atakuja juta kuchezea ndizi kwa maembe ya msimu.

[email protected]

You can share this post!

FATAKI: Ubabe-dume, ujeuri na ujuaji mwingi si ujasiri, ni...

UMBEA: Kile ambacho ni chako, utakipata tu hata kama kipo...