Derby FC kupigana kufa kupona kupanda daraja

Na JOHN KIMWERE

NI kweli wahenga hakupata mafuta kwa mgongo wa chupa walipoketi na kulonga kuwa ‘Lisolokuwapo moyoni pia machoni halipo.’ Ni msemo unaoashiria kwamba hakuna lolote linaloweza kutimia bila ya kufanyiwa kazi.

Aidha unafundisha wanadamu kuwa ili kufikia mafanikio yoyote ni lazima wahusika wazamie mpango mzima kuwawezesha kuibuka na mkakati kabambe bila kuweka katika kaburi la sahau kujiwekea maazimio yote wanayodhamiria kufikia.

Katika anga la michezo msemo huo unahimiza wachezaji kukaza mwendo na kufahamu kiwango wanacho lenga kutimiza kufikia kilele cha mafanikio yao.

Ndivyo wachezaji wa timu ya Derby FC wanavyosadiki. Ingawa ndiyo mwanzo imeanza kupiga ngoma kwenye mechi za Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Tawi la Nairobi Magharibi inalenga kushiriki soka la hadhi ya juu hivi karibuni. Mwenyekiti wake, Wilfred Ongeri maarufu Sam Ongeri anasema kuwa katu hawana jingine bali wamepania kujituma mithili ya mchwa kuhakikisha imefuzu kupandishwa ngazi kushiriki mechi za Ligi ya Kaunti msimu ujao.

”Wanasoka wangu wameanza vyema kampeni za kuwania ubingwa wa Ligi ya Wilaya (Sub County) jambo linalotupatia imani kuwa tunayo fursa ya kufanya vizuri,” mwenyekiti huyo alisema na kutoa wito kwa wahisani wajitokeze na kuungana nao kwenye juhudi za kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi mitaani.

Kocha wa Ngara akiongea na wachezaji wake.

Kwenye utangulizi wa mechi za kipute hicho, Derby FC ilizaba Ngara SportIff FC mabao 3-1. Lamech Bosire alicheka na wavu mara mbili huku Kelvin Ohuru alifunga bao moja. Anasema kuwa matokeo hayo yanaonesha kuwa vijana wake wanaweza kufanya vizuri kwenye kinyang’anyiro hicho.

Naye kocha wake, Benjamin Kyalo anasema ”Sina shaka na wachezaji wangu nina imani tosha watafanya kazi nzuri kwenye kampeni za muhula huu.” Aidha anadokeza kuwa anaamini ana wachezaji wazuri maana wamekuwa wakifanya kweli kwenye mashindano mengine ikiwamo Maisha League Makadara Zone na Moss Foundation League (MFL).

Timu hiyo yenye makazi yake katika eneo la Madakara, jijini Nairobi iliasisiwa na mwenyekiti huyo mtaani Mukuru Kwa Njenga, Nairobi. ”Ni uamuzi niliyofikia nikidhamiria kuzima na kubadilisha mienendo ya vijana kushiriki maovu mitaani kwenye juhudi za kujitafutia riziki,” mwenyekiti huyo akasema.

Klabu hiyo inajumuisha wachezaji kutoka mitaa ya Mukuru Kwa Njenga, Pipeline, South B kati ya mengine katika eneo la Eastlands ambalo huorodheshwa kati ya maeneo yenye idadi kubwa ya visa vya uhalifu katika Kaunti ya Nairobi.

Anasema kwa asilimia kubwa soka limesaidia vijana wengi kujiepusha dhidi ya kushiriki matendo maovu mitaani. Derby FC inajivunia kutwaa ubingwa wa Ligi ya Maisha Kanda ya Makadara 2018 pia ilimaliza ya pili kwenye ngarambe ya Moss Foundation.

Habari zinazohusiana na hii