Ingwe Youth wapania kuoanda ngazi msimu huu

Na JOHN KIMWERE

AFC Leopards Youth imeibuka kati ya timu zinazotifua vumbi la kufa mtu kwenye mechi za Kundi A kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu.

Kikosi hicho cha kocha, Martin Aganda kinajivunia kushinda mechi zote tano ambazo kimeshiriki ambapo tayari kimetwaa uongozi wa kundi hilo katika jedwali kwa kukusanya jumla ya alama 15.

Hata hivyo kundi hilo linatazamiwa kuzua upinzani mkali baina ya washiriki wengine kama Makarios 111 FC (Riruta United), Maafande wa Nairobi Prisons, Amazon Tigers, Kibera Golden FC na Gachie Silver Bullets kati ya zingine.

Kocha huyo anasisitiza kuwa muhula huu wamepania kupambana mwanzo mwisho kuwania tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili.

”Ninaamini wachezaji wangu wameiva pia wanatosha mboga kufanya kweli kwenye mechi za ligi ya msimu huu tunaoshiriki kwa mara tatu mfululizo,” kocha huyo alisema na kutoa wito kwa wachezaji wake wakaze buti kufuata nyayo za wakubwa wao. Kando na hayo pia anasema anataka kuona vijana kadhaa wakitinga viwango vya kuteuliwa kuchezea klabu za Ligi Kuu ya Kenya.

AFC Leopards Youth inajivunia huduma za wachezaji kama beki matata, Edwin Ochieng na Victor ‘Aguero’ Otieno ambao ni wanafunzi wa Shule za Upili. Pia wapo kiungo, Giovanni Lukhumwa, Vincent Nyabuto na Maxwell Otieno ambao wamefaulu kucheka na nyavu mara nane na nne mtawalia.

Kocha huyo anajivunia wachezaji kadhaa waliopitia mikononi mwao na kufanikiwa kuteuliwa kuchezea AFC Leopards inayozidi kutesa kwenye kaampeni za Ligi Kuu muhula huu. Kocha huyo anataja baadhi ya wachezaji ambao wamepitia mikononi mwake kama Vincent Oburu, Austin Odhiambo na Lewis Bandi kati ya wengine.

Anasema analenga kuon amenoa makucha ya wachezaji kama wanne hivi angalau wafanikiwe kujiunga na kikosi cha wakomavu -AFC Leopards kushiriki mechi za Ligi Kuu (BKPL) msimu ujao.

”Bila kujipigia debe hilo ndilo tumaini langu ambapo hatua hiyo itachangia wengine kukaza buti na kuwapa motisha zaidi,” alisema na kuongeza kuwa kwa makocha nyakati zote furaha yao huwa kukuza wachezaji na kusonga mbele.

AFC Leopards ilianza kushiriki kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) mwaka 2018. Ilifanikiwa kujikatia tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki mechi NWRL mwaka 2017 baada ya kushiriki mechi za Ligi ya Kaunti ndani ya misimu miwili.

Habari zinazohusiana na hii