Modern Coast Yazidi Kudidimia Supaligi ya Taifa

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

TIMU ya Mount Kenya United FC ilijihakikishia imerudi kwao nyumbani na pointi zote tatu za Supaligi ya Taifa ilipoifunga Modern Coast Rangers FC kwa mabao 2-1 kwenye mechi iliyochezwa uwanja wa Serani.

Katika pambano hilo lilokuwa la kuvutia ambalo hata hivyo lilikosa mashabiki ambao hawaruhusiwi kushuhudia kutokana na kujikinga na Covid-19, timu ya wageni ya Mount Kenya ilichukua uongozi wa mapema Felix Ouma alipotingisha nyavu dakika ya 10.

Katika kipindi cha pili, Rangers ilijikakamua dakika tano za mwanzo lakini washambuolizi wake walikosa nafasi mbili za kusawazisha. Mount Kenya ikajipatia bao lao la pili kunako dakika ya 55 mfungaji akiwa Kevin Ndung’u.

Kuanzia hapo, Ranges iliutawala mchezo na katika dakika ya 64, George Owiti akaipatia timu hiyo bao la kufuta machozi. Ingawa Rangers iliendelea kutawala mchezo, mabeki wa Mount Kenya hawakutoa upenyo.

Kocha wa Mount Kenya, Thomas Okongo alitamba kuwa ushindi wake huo ni wa kujivunia kwani wameweza kubeba pointi zote sita kutoka kwa timu za Mombasa kutokana na awali kuwachapa Coast Stima kwa idadi kama hiyo ya mabao 2-1.

“Ningependa kujivunia kazi iliyofanywa na wanasoka wangu kwani wamehakikisha tumeziadhibu timu za Mombasa na kuchukua alama zote sita. Nina imani tunaweza kumaliza ligi hii katika nafasi tatu za juu,” akasema Okongo.

Naye mkufunzi wa Rangers, Mohamed Ahmed Mohaa alisema kutokana na mabadiliko ya kuwa na wachezaji wapya, watafanya bidii kuhakikisha wameingiliana na wachezaji walioko hapo awali. “Tutarekebisha makosa na tutafanya vizuri mechi zijazo,” akasema Mohaa.

Habari zinazohusiana na hii