• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Kilifi Ladies FC Yaanzishwa Kuwasaidia Wasichana Wajiepushe Na Mimba Za Mapema

Kilifi Ladies FC Yaanzishwa Kuwasaidia Wasichana Wajiepushe Na Mimba Za Mapema

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

KAUNTI ya Kilifi ni mojawapo ya zile ambazo zimefahamika kuwa na wasichana wengi wanaojihusisha na mimba za mapema na nyendo nyingine potofu zikiwemo utumizi wa mihadharati kati ya maovu mengine.

Katika juhudi za kuondoa ama kupunguza tabia hizo, wakazi wanne wa Kaunti ya Kilifi walikutana kuanzisha rasmi timu ya soka ya Kilifi Ladies FC ambayo ina wachezaji kutoka sehemu mbalimbali za kaunti hiyo.

Sababu kubwa iliyowafanya watu hao wakiongozwa na Bendera Wilson Charo ambaye ni mfadhili mkuu, meneja wa timu hiyo Anthony Kadenge, Mjumbe Samson Menza na Kocha Shafi Said ni kuhakikisha wasichana wa kaunti hiyo wanaendeleza vipaji vya uchezaji wao.

Bendera amesema walipokutana walifahamu kuweko kwa umuhimu wa klabu ya soka la wanawake ya Kilifi Ladies FC kuanzishwa kama njia mojawapo muhimu ya kuwafanya wasichana na wajiepushe na maovu huku wakijihusisha kikamilifu kuinua vipaji vya uchezaji wao.

“Tulainzisha klabu ya Kilifi Ladies kuwasaidia wasichana wenye vipaji kutambulika na kujiepusha na mimba za mapema na tabia potofu zikiwemo utumiaji wa mihadharati na vitendo vingine visivyokuwa na maana,” akasema Bendera.

Aliwashukuru baadhi ya wahisani waliojitolea kuhakikisha klabu hiyo inajimudu na inaweza kuendelea kwa sababu ni ya wasichana wa kaunti yote ya Kilifi. Kutokana na udhamini wa wahisani, iliweza kuzunguka sehemu zote za Pwani kucheza mechi za kirafiki.

Bendera aliwashukuru wadhamini hao kwa msada waliowapa. Hao ni Mombasa Cement, Project 720, Coast Value, Hotel Titanic, Wakili George Kithi, Mama Naomi Cidi na Mama Margaret Kahara.

Alisema kutokana na kupata ushindi huo, ni dhahiri kuwa kuna talanta katika kaunti hiyo na hivyo wameona waihifadhi klabu hiyo ili iweze kujitayarisha kwa ligi ikiwezekana waanzie Ligi ya jimbo la Pwani.

“Tumeona jinsi ya timu yetu hii inavyoendelea vizuri na hivyo, tutawasiliana na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ituchagulie ligi ya kushiriki. Tunaamini tunaweza kushiriki ligi yoyote tutakayopewa nafasi,” akasema mfadhili huyo.

Kocha Samson Jumbe anasema wachezaji wake wana vipaji ambao ana uhakika muda usiokuwa mrefu, watavutia maskauti wa klabu kubwa nchini na ana imani wakuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Harambee Starlets wakiwaona, watawateua baadhi kwenye kikosi cha timu hiyo.

Alisema walianza ziara zao katika Kaunti ya Mombasa ambapo iiishinda Changamwe Ladies kwa mabao 5-4 wakarudi nyumbani Kilifi ambapo ikawachapa Kaloleni Queens 5-2 kabla ya kuelekea Taita Taveta ambapo ikaikung’uta Crown Ladies 4-1.

Halafu ikaelekea huko Kwale ambapo ilifanikiwa kuichabanga Ukunda Starlets kwa mabao 4-0, ikaelekea huko Kaunti ya Lamu ikaweza kuibebesha kapu la mabao 8-0 timu ya Uhuru Queens FC.

Ikafika Tana River na kuishinda Galole Ladies 2-1 kabla ya kurudi nyumbani Kilifi ambako ilifanikiwa kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Msato Starlets na ushindi mwingine wa 1-0 dhidi ya wageni wao kutoka Mombasa, Changamwe Ladies.

Nahodha wa kikosi hicho cha Kilifi Ladies FC, Nancy Mweni ametoa shukrani nyingi kwa waanzilishi wao na kwa jinsi wanavyowafanyia mipango ya kujipa mazoezi yanayowafaa na ambayo yanawafanya waweze kushinda mechi zao zote.

“Nina imani kubwa nikiwa na wenzangu, tutajitahidi kuhakikisha tunafika mbali kisoka,” akasema Nancy.

Wanasoka wengine wa kikosi hicho ni Sophia Garama, Victoria Masha, Risper Sidi, Everlyne Jomo, Emily Sammy, Naomi Kenga, Joan David, Judith Zawadi, Wakesho Ruma, Fatuma Kahindi, Everlyne Zawadi, Pato Tsutsu, Purity Karembo, Juliana Julius, Esther Njeri, Salma Omar na Caroline Achieng.

You can share this post!

Modern Coast Yazidi Kudidimia Supaligi ya Taifa

Dkt Ruto asema ni kufa kupona Harambee Stars ikikwaana na...