• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
TAHARIRI: Heko kwa Harambee Stars kujikaza kisabuni

TAHARIRI: Heko kwa Harambee Stars kujikaza kisabuni

KITENGO CHA UHARIRI

LICHA ya timu ya taifa ya soka, Harambee Stars, kubanduliwa nje ya kombe la Taifa Bingwa Afrika (AFCON) 2022 vijana wa nyumbani walionyesha mchezo mzuri katika sare ya 1-1 dhidi ya Misri, mnamo Ijumaa.

Ni mechi iliyowaweka kwenye mizani kali ikizingatiwa ilikuwa ya kufa kupona; tena dhidi ya mabingwa hao mara saba wa AFCON ambao walikuwa na mvamizi matata Mohamed Salah wa klabu ya Liverpool nchini Uingereza.

Hata baada ya kufinywa bao la mapema Ijumaa usiku uwanjani Kasarani, Nairobi, vijana wa kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee hawakunywea. Walijikaza kisabuni na kutinga goli la kusawazisha zikiwa zimesalia dakika 25 kabla mechi kuisha.

Kilichojitokeza zaidi ni kwamba Stars walipoteza nafasi muhimu walizopata dhidi ya Misri. Wangalitumia fursa hizo kufunga bao la pili au zaidi, wangalikuwa na mwanya katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Togo mwezi huu; na hivyo kuweka hai matumaini ya kushiriki AFCON kwa mwaka wa pili mfululizo.

Sasa watakuwa tu mashabiki katika makala yajayo nchini Cameroon mnamo 2022.

Yote tisa, suala lingine linalojitokeza ni kwamba kichapo cha 2-1 ugenini kutoka kwa wanavisiwa wa Comoros, ndicho kiliyumbisha zaidi mashua ya Kenya.

Hii ukijumuisha sare tatu mfululizo za 1-1 katika mechi za ufunguzi Kundi G, mbili zikiwa nyumbani. Ni sare ambazo zilinyima kikosi cha taifa alama muhimu; sembuse mabao ambayo yangewasaidia iwapo wangetoshana pointi na wapinzani wao Misri, Comoros na Togo.

Katika mashindano ya muondoano, timu lazima itumie uga wa nyumbani kupata alama zote liwe liwalo.

Pili, mechi zote huwa sawa na fainali ya kombe; hakuna timu nyonge wala mechi rahisi. Ndiposa limbukeni Comoros wamefuzu kwa AFCON 2022 baada ya kunyakua nafasi ya pili kundini.

Wameshinda mechi mbili na kukabana mbili hadi kufikia sasa; sawa na miamba Misri ila wana Pharao wanawazidi kwa tofauti ya magoli.

Sasa Shirikisho la Soka (FKF) na benchi ya kiufundi ya Harambee Stars zianze kupangia makala yatakayofuata; wakitilia maanani mahesabu yatakayowezesha Stars kuvuna pointi zote tatu katika mechi za nyumbani, na angalau kule ugenini watoke sare ya magoli mengi.

ugenini.

Mvamizi matata wa Harambee Stars Michael ‘Engineer’ Olunga alisherehekea kugonga umri wa miaka 27 hapo jana akikiri alipoteza nafasi nyingi muhimu dhidi ya Misri siku iliyotangulia ugani Kasarani.

Vijana Jacob ‘Ghost’ Mulee walikabwa 1-1 katika mchuano huo wa Kundi G wa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2022 na kubanduliwa.

Katika mechi hiyo ambayo Magdy Afsha aliweka Mafirauni kifua mbele 1-0 dakika ya pili naye Abdalla Hassan akasawazishia wenyeji dakika ya 65, Olunga alipoteza nafasi kadhaa huku bao la Masud Juma likikataliwa.

“Tulipoteza nafasi kadhaa nzuri jana (Machi 25), lakini najivunia jinsi timu ilijinyanyua baada ya kutikiswa na bao la mapema,” alisema mshambuliaji huyo wa Al Duhail inayoshiriki Ligi Kuu ya Qatar.

“Heko Erick ‘Marcelo’ Ouma na Daniel Sakari kwa kazi nzuri,” aliongeza kuhusu mabeki hao.

Misri na Comoros, ambayo ilitoka 0-0 dhidi ya Togo nchini Comoros hapo Alhamisi, zilijikatia tiketi ya kuwa AFCON2022 nchini Cameroon kutoka kundi hilo. Zina alama tisa baada ya kujibwaga uwanjani mara tano. Kenya ina alama nne nayo Togo ni ya mwisho kwa alama mbili.

Wakenya wengi walipongeza Stars kwa kuonyesha mchezo mzuri dhidi ya Misri iliyokuwa na nyota Mohamed Salah, licha ya kuwa Stars itakuwa tu shabiki katika makala yajayo ya dimba hilo.

Washika dau na mashabiki wa soka kutoka Pwani Walipongeza Mulee kwa kuweka imani yake kumchezesha mfungaji wa bao la Kenya, Hassan kutoka Bandari FC.

Walikuwa na hamu kubwa kuona Hassan na Danson Namasaka kutoka klabu hiyo wakichezeshwa, ingawa Hassan pekee ndiye alipata fursa.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC, Aref Baghazally alisema wamekuwa na hamu ya muda mrefu kushuhudia wachezaji wao wakipangwa kikosini. Alisema kuwa kuchezeshwa kwa Hassan na kufunga, kumedhihirisha kuwa Pwani kuna wanasoka wenye kuaminika wakiwa uwanjani.

Alipendekeza baada ya kibarua cha Togo, Mulee atembelee eneo hilo kushuhudia mechi za Ligi ya Supa pamoja nyinginezo.

“Nina uhakika akizuru Pwani, atapendezwa na vipaji vilivyoko na kupata wanasoka kadhaa wa kujaribu katika timu ya taifa. Tunataka timu ichaguliwe kutokana na wanasoka wazuri na wala si kutoka kwa klabu zenye majina,” akasema Baghazally.

You can share this post!

Suluhu atoa hongera kwa raia kwa uzalendo mkuu

MUTUA: Suluhu aponye madonda aliyoacha Rais Magufuli