• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
NDIVYO SIVYO: Bandubandu huisha gogo na chovyachovya humaliza buyu la asali haziwiani kimaana

NDIVYO SIVYO: Bandubandu huisha gogo na chovyachovya humaliza buyu la asali haziwiani kimaana

Na ENOCK NYARIKI

MAKALA haya yataziangazia methali mbili ambazo mara nyingi hudhaniwa kuwa na maana sawa.

Methali hizo ni: Bandubandu huisha gogo na Chovyachovya humaliza buyu la asali. Juzi nilipomweleza bwana fulani kuwa nilikuwa nimedhamiria kuifanya kidogokidogo kazi niliyokuwa nayo mpaka niikamilishe, aliniambia, “Vyema. Unajua chovyachovya humaliza buyu la asali.”

Matumizi ya methali hiyo katika muktadha huo wa mazungumzo hayakuwa sahihi. Nitaifafanua kauli hii baadaye ila ni muhimu kutaja kuwa yapo mambo kadha ambayo huwafanya watu kudhani kuwa methali mbili tulizozitanguliza katika mjadala wetu ni sawa kimaana.

Jambo la kwanza linatokana na umbo la nje la methali zenyewe. Kwa kutaja umbo la nje ninamaanisha mpangilio wa maneno kwenye methali zenyewe. Mathalani, maneno “huisha’’ na “humaliza” yana maana sawa. Toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu linalifafanua neno isha kuwa kufika mwisho wa kitu au jambo. Maneno malizika na koma yanaorodheshwa kama visawe vya neno hilo. Jambo hili linatudokezea kuwa maneno hayo mawili yanaweza kutumiwa kwa njia sawa.

Pili, kujitokeza kwa dhana ya kutoa katika maana za ndani za methali hizo. Katika methali ‘Bandubandu huisha gogo’ kuna wazo la kupunguza gogo kubwa kwa kubandua kipande kidogo kidogo. Aidha, katika methali ‘Chovyachovya humaliza buyu la asali’ kuna wazo la kumaliza asali kwa kitendo cha kutumbukiza kidole ndani ya buyu la asali. Ni sahihi kusema kwamba dhana ya kutoa au kupunguza inawasilishwa na maneno isha na maliza ambayo pia yanazipamba methali hizo kwa nje.

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa methali hizi mbili zinawasilisha maana mbili tofauti kabisa. Maana hizi zinawasilishwa kupitia dhima ya methali.

Methali ‘Bandubandu huisha gogo’ inahimiza kuhusu umuhimu wa kujitahidi kuipunguza kazi au shughuli ambayo inaonekana kuwa kubwa kwa kuifanya kidogokidogo hadi iishe. Kwa upande mwingine ‘Chovyachovya humaliza buyu la asali inatahadharisha dhidi ya tabia ya kutumia ovyo au kwa ubadhirifu mali au kitu chochote alicho nacho mtu kwa sababu wakati atakapopiga hamadi, kitakuwa kimeisha.

Alhasili, ‘Bandubandu huisha gogo’ inawahimiza watu kutolalamikia ukubwa wa kazi au shughuli kwa sababu wakiifanya kidogokidogo na kwa subira, mwishowe itakamilika. Hii ndiyo methali ambayo bwana niliyemtaja katika sehemu fulani ya makala haya angeitumia katika usemi wake.

Methali ‘Chovyachovya humaliza buyu la asali nayo huwatahadharisha watu dhidi ya vishawishi vya kutumia kidogokidogo mali waliyo nayo kwa shughuli ambayo si muhimu kwa sababu mali yanayoonekana kuwa mengi yanapotumiwa ovyo hatimaye huisha.

You can share this post!

NASAHA: Mwandalie mwanao jukwaa la kuyaratibu malengo yake...

Mwili wa aliyemuuza ng’ombe Sh130,000 wapatikana...