• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Muungano wa makanisa chini ya mwavuli wa FEICCK walaani kitendo cha polisi kuvamia kanisa

Muungano wa makanisa chini ya mwavuli wa FEICCK walaani kitendo cha polisi kuvamia kanisa

Na LAWRENCE ONGARO

MUUNGANO wa makanisa wa Federation of Evangelical and Indigenous Christian Church of Kenya (FEICCK) umeshutumu hatua ya polisi kuvamia kanisa na kufurusha waumini mwishoni mwa wiki jana.

FEICCK imeitaka serikali iwachukulie hatua wote waliohusika na kitendo hicho kwani inadai kuwa kanisa ni mahali patakatifu ambapo ni sharti kuheshimiwa.

Wakiongozwa na Askofu wa kanisa la Glory Outreach Assembley Bw David Munyiri wachungaji hao walisema kitendo hicho ni cha kulaumiwa kwa sababu “nyumba ya Mungu ni mahali patakatifu panapostahili heshima kuu.”

Kwa kauli moja wachungaji wamelaani kitendo hicho wakikitaja kama cha ukatili na kwamba “hatufai kushuhudia kitendo kama hicho ikizingatiwa tulijinyakulia uhuru miaka 58 iliyopita.”

Walieleza ya kwamba kanisa halina ubaya wowote na serikali na kwa hivyo pande zote mbili zinastahili kufanya kazi kwa umoja bila mkwaruzano.

Walizidi kueleza ya kwamba wamekuwa wakifuata maagizo yote ya kiafya ili kukabiliana na Covid-19.

Walisema uhuru wa kuabudu unastahili kuwepo.

“Sisi kama wachungaji tunafuata sheria zote zilizowekwa na Wizara ya Afya na kwa hivyo kama kuna jambo linaloweza kuleta mvutano ni vyema kulitatua kwa njia ya uelewano,” alisema Askofu Munyiri.

Kwa niaba ya wachungaji wenzake alisema watafanya juhudi kuona ya kwamba wanawashauri waumini wao kufuata sheria za kuzuia kuenea kwa Covid-19, hasa kuvalia barakoa, kunawa mikono na kuweka nafasi ya zaidi ya mita moja kati ya mtu mmoja na mwingine.

Alizidi kueleza kuwa kila mara kanisa linahubiri amani na kwa hivyo hawangetaka kuharibu uhusiano na serikali.

Wanaiomba serikali kufungua shughuli za kawaida ili wananchi waweze kuendeleza maisha yao ya kawaida.

Hivi majuzi serikali ilifunga kuingia kaunti tano ambazo ni Nairobi, Kiambu, Machakos, Kajiado na Nakuru hatua iliyoyumbisha biashara kadhaa.

Maabadi katika kaunti hizo yamewekewa vikwazo vya kushirikisha waumini wachache kwenye maombi yao.

Hatua hiyo pia imesababisha makanisa kadha kuendesha maombi yao kupitia mitandao.

You can share this post!

Bunge la kaunti lafungwa kuepusha ueneaji corona

Zeddie Lukoye awasilisha barua Waislamu wamsamehe kwa...