Vigogo wapimana akili

Na BENSON MATHEKA

VIGOGO wa kisiasa nchini wanaendeleza njama zinazoweza tu kufananishwa na kuchezeana karata ya patapotea, kila mmoja akijaribu kumshinda maarifa mwenzake hasa kuhusu miungano wanayolenga au wanayopendelea kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Rais Uhuru Kenyatta anaonekana kumcheza kinara mwenzake katika handisheki, Raila Odinga, ikidaiwa kiongozi wa nchi anapendelea muungano wa One Kenya Alliance unaoshirikisha vyama vya Wiper cha Kalonzo Musyoka, Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha Moses Wetangula na Kanu cha Seneta wa Baringo Gideon Moi.

Kulingana na wadadisi, hali hii imemsukuma Bw Odinga kufanya mazungumzo na Naibu Rais William Ruto kupitia kwa wandani wake ikisemekana ni kwa lengo la kumdhihirishia Rais Kenyatta kwamba, angali mbabe wa siasa nchini anayeweza kufanya maamuzi yasiyoweza kutarajiwa.

Handisheki ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, ilionekana kuwa ya kumnyima Dkt Ruto nafasi ya kuingia ikulu.Rais Kenyatta na Dkt Ruto wametofautiana vikali na licha ya kusema kwamba ni Mungu anayeamua viongozi na kumtenga Dkt Ruto serikalini, Rais Kenyatta hajawahi kutangaza hadharani kwamba hatamuunga naibu wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“ODM inaamini kwamba kuna njama pana ya kumzuia Bw Odinga kuingia ikulu inayopendekezwa na watu walio karibu sana na Mamlaka na hatulali. Chama chetu ndicho kikubwa nchini kwa sasa baada ya Jubilee kuporomoka na tuna uwezo wa kusahau ya kale na kubuni muungano utakaotikisa Kenya,” asema mbunge mmoja wa ODM ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Mnamo Jumatano wiki iliyopita, ilibainika kuwa Bw Odinga na Dkt Ruto wamekuwa wakirushiana chambo baada ya Gavana wa Kakamega kukutana na Naibu Rais eneo la Narok na siku iliyofuata, akawasilisha ripoti kwa Bw Odinga jijini Nairobi.

Hii ilikuwa ni wiki moja baada ya Bw Odinga kuonekana pamoja na Rais wakikagua miradi ya maendeleo jijini Nairobi, hatua ambayo wadadisi walisema ililenga kumtuliza kiongozi huyo wa chama cha ODM asiungane na Dkt Ruto.Duru zinasema kwamba, baada ya Rais kubaini kwamba Odinga alikuwa amemtuma Oparanya kukutana na Dkt Ruto, Rais Kenyatta alimpigia simu.

Wachanganuzi wanasema kuna kila dalili za njama ya kuvuruga ngome za Bw Odinga za Magharibi na Pwani ili kumnyima ushawishi wa kumwezesha kuunda muungano thabiti unaoweza kukabili One Kenya Alliance.

Hata hivyo, katika muungano huo wa One Kenya Alliance, hakuna uwazi kuhusu mipango ya vigogo husika kwani kila mmoja anasisitiza atawania urais.

Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, haitashangaza kwamba viongozi hao huonekana pamoja mchana ilhali usiku wanaenda kushauriana na wengine kuhusu miungano mingine.

“Kuna ujanja mwingi unaoendea miongoni mwa vigogo wa kisiasa kuhusu 2022. Hali halisi itabainika kuanzia Agosti mwaka huu. Kwa sasa, vigogo wa siasa wanapimana akili na hata nguvu za ufuasi,” asema mdadisi wa siasa Simon Waruinge.

Matamshi ya Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kwamba ODM, inapanga muungano hata kama itakuwa na mahasimu wake wa kisiasa, yalizidisha mdahalo kuhusu muungano wa Bw Odinga na Dkt Ruto.

Inasemekana Dkt Ruto anacheza kivyake licha ya kunuia kuunda muungano wa kisiasa ikiwa ni pamoja na ODM.Ingawa baadhi ya washirika wake wanaunga muungano wake na Bw Odinga kukabili One Kenya Alliance, duru zinasema anashuku waziri mkuu huyo wa zamani kufuatia ukuruba wake na Rais Kenyatta.

Washirika wake hasa wa kutoka Mlima Kenya ambako amejenga umaarufu wamemshauri kwamba kuungana na Bw Odinga kutamkosesha kura za eneo hilo.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Martin Andati, kwa kurushia Ruto chambo, Bw Odinga anataka kutia hofu washirika wake katika muungano wa NASA ambao wako katika One Kenya Alliance na pia kinara mwenzake katika handisheki.

Hata hivyo mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri anasema kwamba Dkt Ruto hana nia ya kuungana na Bw Odinga ishara kwamba anampima akili.Lakini Bw Waruinge anasisitiza kuwa kinachoendelea kwa sasa ni kupimana ujanja kabla ya miungano itakayobadilisha mkondo wa siasa nchini.

Habari zinazohusiana na hii

Mradi wa Uhuru 2022