• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Mwalimu Mkuu alivyojitoa mhanga kufanikisha elimu

Mwalimu Mkuu alivyojitoa mhanga kufanikisha elimu

Na WYCLIFFE NYABERI

MWALIMU Mkuu wa shule ya kutwa ya Sosiana iliyo Transmara Mashariki, Kaunti ya Narok, Bi Margret Njoki, amekuwa akitembea zaidi ya kilomita 20 kila siku ili kufanikisha Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) kwa wanafunzi wake.

Sababu za kutembea kwake si kwamba hakuna magari wala pikipiki ambazo zingerahisisha uchukuzi, bali hakuna barabara yoyote inayofika shuleni.

Huku maeneo mengi nchini yakishamiri barabara nzuri zilizojengwa hadi vitongojini kufuatia ujio wa ugatuzi, hilo kwa wakazi wa Sosiana limebaki kuwa ndoto tu.

Masaibu ya Bi Njoki ni mfano mzuri wa changamoto wanazozipitia walimu wakuu, maafisa wa polisi na wale waliopewa wajibu wa kufanikisha KCSE inayokaribia kutamatika.

Amekuwa akitaabika na wenzake kwa kupitia vichochoroni, kupanda vilima vidogo vilivyojaa miiba na wakati mwingine hata kuhatarisha maisha yao wanapovuka kijito kilichoko sehemu hizo, ambacho hujaa maji wakati wa mvua nyingi.

Bi Njoki na walimu wengine huchukua karatasi za mtihani wa KCSE kila alfajiri kutoka mji wa Emurua Dikirr, ambako ndiko kuliko sanduku la kuhifadhi mtihani wa shule za eneo hilo.

Akishapokezwa mtihani huo, yeye huabiri gari na maafisa wengine linalowaleta hadi sehemu iitwayo Tinga ya Mama na hapo ndio safari yao ya kutembea huanza.

“Hapo huwa ni majira ya karibu saa kumi na mbili na nusu asubuhi. Safari yetu hutuchukua takribani saa moja kufika shuleni. Kutoka Kwa Tinga ya Mama hadi shuleni ni kilomita kumi na tunaporudisha karatasi za wanafunzi, tunatembea zingine kumi. Hayo ndiyo maisha yetu kwa sasa,” akasema mwalimu huyo.

Tangu mtihani uanze hakuna hata siku moja wamechelewa kuufikisha shuleni kwa wakati ufaao.

Kulingana na Bi Njoki, siku ya kwanza kabisa mtihani huo ulipoanza ilikuwa kibarua kigumu kwake lakini kwa sasa amezoea na hapati maumivu ya uchovu tena.

“Nimepoteza uzani kwa kutembea huku hadi wanafunzi wangu wameniambia hilo. Kukinyesha huwezi kutembea na viatu vya kawaida. Niliwaeleza wanafunzi kuwa iwapo nitapoteza uzani wangu na wao wapite mitihani, hiyo itakuwa furaha yangu milele,” akatabasamu Bi Njoki.

Mwalimu huyo alipata uhamisho kwenda Sosiana Januari mwaka huu baada ya mwalimu mwingine kukataa kufanya kazi shuleni humo kwa kutoyapenda mazingara hayo ya kazi.

“Nilitumwa hapa baada ya aliyekuwa aichukue nafasi hii kutorudi tena baada ya kuripoti siku ya kwanza. Nilitokea Kajiado lakini mimi ni mzawa wa Nyeri. Wenzangu walinieleza kwamba mwalimu huyo alipowasili, alitamaushwa na ukosefu wa barabara nzuri ya kusaidia usafiri na ukosefu wa vifaa vingine shuleni,” akaongeza mwalimu huyo.

Shule ya Sosiana ina idadi ya wanafunzi 125 na 23 ni watahiniwa wa mwaka huu. Ilianzishwa mwaka wa 2015 na miundo msingi ni haba.

Madarasa ni manne tu na imebidi walimu kugawanya darasa la kidato cha pili ili iwasitiri mwalimu mkuu, naibu wake na karani wa shule kwa kuwa maabara waliyokuwa wakiyatumia kama afisi zao yanatumiwa na wanafunzi kufanyia mtihani.

Ni katika darasa hilo pia ambapo wametengeneza maktaba ndogo kwa faida ya wanafunzi wanaodurusu mtihani wao ukiendelea.

Nguvu za umeme pia hazijafika shuleni lakini nyaya za stima tayari zimewekwa.

Wakazi wa Sosiana wametoa wito kwa viongozi wa eneo hilo na serikali kuingilia kati na kuwatengenezea barabara nzuri itakayofungua kitongoji chao.

You can share this post!

Gharama ya juu ya matibabu inavyobagua maskini

Uganda kuanza kuuza mafuta 2025