• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
WARUI: Matokeo ya mtihani wa KCPE yanazua maswali kadhaa

WARUI: Matokeo ya mtihani wa KCPE yanazua maswali kadhaa

Na WANTO WARUI

MATOKEO ya mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane, KCPE, yaliyotolewa wiki jana yalipokelewa nchini kwa kwa njia tofauti tofauti.

Kuna wale walioyapokea kwa shangwe na vigelegele, wengine kwa huzuni na kutamauka na wengine kwa shauku na kutoamini.

Akitangaza matokeo hayo, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha alisema kuwa wanafunzi hao wa mwaka wa 2020, walifanya vizuri zaidi wakilinganishwa na wale wa mwaka wa 2019 licha ya changamoto zilizokuwapo za ugonjwa wa Covid-19.

Maneno haya yalikuwa ya kutia moyo ikikumbukwa kuwa wanafunzi hawa walikuwa wamekaa nyumbani kwa muda wa miezi saba bila masomo.

Zaidi ya hayo, aliweza kudokezea kuwa shule za umma zilifanya vyema zaidi zikilinganishwa na zile za kibinafsi. Alisema kuwa kati ya wanafunzi kumi na watano bora nchini, kumi walikuwa wametoka katika shule za umma na watano pekee walitoka katika shule za kibinafsi. Hata hao watano waliotoka shule za kibinafsi hawakuchukua nafasi za kwanza nchini.

Kwa mtazamo tu, Waziri alionyesha wazi kuwa shule za umma ni bora zaidi na zinafanya vyema kuliko zile za kibinafsi jambo ambalo wananchi wengi wanapinga.

Matokeo ambayo yalipokelewa na wanafunzi wengi kutoka shule bora za kibinafsi nchini yalikuwa ya kutamausha. Maswali kadha wa kadha yanajitokeza ambayo yanahitaji majibu.

Je, ni kweli kuwa shule za umma zimekuwa bora zaidi ya zile za kibinafsi? Je, matokeo haya ya mwaka huu ‘yalionea’ shule za kibinafsi? Na kama ndivyo hivyo, sababu yake ni gani? Je, mwanafunzi anayesomea shule ya kibinafsi ana haki yake sawa na yule anayesomea shule ya umma au kuna yule ana haki zaidi? Je, walimu na vifaa bora vinavyopatikana katika shule za kibinafsi ni kosa la mwanafunzi anayesomea huko?

Mara kwa mara, serikali imekuwa ikisema kuwa wanafunzi wote ni sawa licha ya pale wanaposomea. Ikiwa ni hivyo, pana haja sana ya wanafunzi wote watendewe haki licha ya mazingira waliyomo. Hakuna mwanafunzi ambaye huchagua kuzaliwa katika familia ya kitajiri au yenye umaskini – haya huwa ni majaliwa tu. Katika kuwapokeza wanafunzi wote matokeo, ni muhimu kila mwanafunzi kuhisi kuwa alipata alama alizotolea jasho.

Inapofika kuwa matokeo ya mitihani ya kitaifa yanatiliwa shaka, basi jambo kama hilo linaweza kuleta utengano dhidi ya wahusika na wananchi kwa ujumla. Ama kwa hakika, mzazi aliyejitoa mhanga na kujinyima ili angalau aone mtoto wake amefaulu masomoni atashangaa sana ikiwa haki haikutendeka kwa mwanawe.

Kwa wale wote waliofanya mtihani wa KCPE, Taifa Leo inawapa heko kwa matokeo bora.

You can share this post!

TAHARIRI: Unyama wa polisi si dawa ya corona

ONYANGO: Serikali irejeshe shuleni waliokosa kufanya KCPE