• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
ONYANGO: Serikali irejeshe shuleni waliokosa kufanya KCPE

ONYANGO: Serikali irejeshe shuleni waliokosa kufanya KCPE

Na LEONARD ONYANGO

KAULI ya Waziri wa Elimu George Magoha ambapo alipuuzilia mbali watahiniwa 12,424 waliokosa kufanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka huu inafaa kushutumiwa.

Alipokuwa akitangaza matokeo ya KCPE Alhamisi, Prof Magoha alisema kwamba watahiniwa 12,424 kati ya milioni 1.2 waliojisajili kufanya mtihani huo, si kitu na haifai kushtua Wakenya.

Waziri Magoha alisema kuwa katika mtihani wa 2019, watahiniwa 8,000, walikosa kufanya mtihani wa KCPE. Hivyo, mwaka huu kulikuwa na ongezeko la watahiniwa wasiozidi 5,000.

Alipongeza machifu na viongozi wengine wa serikali kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanarejea shuleni baada ya kukaa nyumbani kwa zaidi ya miezi minane kufuatia mlipuko wa janga la virusi vya corona.

Kwanza kabisa, Prof Magoha alipotosha Wakenya kwa kudai kwamba wanafunzi 8,000 walikosa kufanya mtihani wa KCPE 2019.

Ukweli ni kwamba ni watahiniwa 5,530 waliokosa kufanya mtihani mwaka huo. Hiyo inamaanisha kuwa kulikuwa na ongezeko la watahiniwa 7,894 ambao hawakujitokeza kufanya mtihani wa KCPE mwaka huu.

Mwaka ambapo watahiniwa 8,347 walikosa kufanya mtihani ilikuwa 2018.

Kuna uwezekano kwamba sehemu ndogo ya watahiniwa waliokosa kujitokeza kufanya mtihani wao walifariki au wazazi wao walihamia katika maeneo ya mbali haswa miongoni mwa jamii za kuhamahama.

Lakini idadi kubwa ya watahiniwa hao walioolewa, walioa au walioachana na shule na kujitosa katika shughuli za kutafuta biashara kama vile bodaboda, uvuvi kati ya nyinginezo.

Wakati wa likizo ndefu, mwaka jana, kulikuwa na shughuli tele za kuwapasha tohara vijana na huenda baadhi yao walihisi kuwa watu wazima wakaachana na shule.

Vilevile, inawezekana kwamba baadhi ya wasichana waliokuwa wamejisajili kwa ajili ya KCPE waliolewa wakati wa likizo ndefu.

Ni jambo la kusikitisha kwamba kila mwaka maelfu ya watahiniwa wanakosa kujitokeza kufanya mitihani yao lakini serikali inaliona kuwa jambo la kawaida. Hakuna hatua zinazochukuliwa.

Ikiwa watahiniwa zaidi ya 12,000 walikosa kujitokeza kufanya mtihani wao wa KCPE, kuna uwezekano mkubwa kwamba maelfu ya wanafunzi wa madarasa ya chini pia hawakurejea shuleni baada ya shule kufunguliwa Januari, mwaka huu.

Serikali haina budi kuanzisha uchunguzi kubaini waliko watahiniwa hao. Ni jukumu la serikali kurejesha shuleni wasichana walioolewa kabla ya kufanya mtihani wao.

Watoto waliokosa kufanya mtihani kwa sababu wazazi wao walihama nao katika jamii za kuhamahama, wanafaa kusaidiwa kurejea shuleni.

Watoto walioacha shule na kujitosa katika huduma za bodaboda, uvuvi na biashara nyinginezo wanastahili kurejeshwa shuleni.

Serikali pia ianzishe juhudi za kusaka wanafunzi wa madarasa ya chini waliokosa kurejea shuleni baada ya likizo ndefu iliyosababishwa na janga la corona.

You can share this post!

WARUI: Matokeo ya mtihani wa KCPE yanazua maswali kadhaa

DIMBA: Huyu Vitinha wa Wolves kama ferari, akitoka unyoya...