• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
SHINA LA UHAI: Dhiki ya wagonjwa huku vikwazo vya Covid vikiathiri matibabu ya kifua kikuu

SHINA LA UHAI: Dhiki ya wagonjwa huku vikwazo vya Covid vikiathiri matibabu ya kifua kikuu

Na PAULINE ONGAJI

MARADHI ya Covid 19 yalipochipuka, mataifa mengi, Kenya miongoni mwao, yalipiga marufuku usafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine, kama mbinu ya kudhibiti ugonjwa huu.

Amri hii iliathiri watu wanaokumbwa na matatizo mbali mbali ya kiafya. Wagonjwa wa maradhi ya kifua kikuu (TB) nchini, hawakusazwa.

Mbali na huduma za hospitali kuathirika, baadhi ya vituo vya kimatibabu vilibadilishwa na kutengewa waathiriwa wa Covid-19. Aidha, baadhi ya wagonjwa wa TB walikumbwa na hofu ya kuambukizwa maradhi ya Covid-19, na hivyo wakaamua kususia kwenda hospitalini.

Kwa baadhi yao, matatizo ya kiuchumi — kama vile kukosa pesa za kununua chakula, na nauli ya hospitalini – yaliyosababishwa na athari zilizoambatana na maradhi ya Covid-19, yalifanya maisha kwao kuwa magumu sana.

Isitoshe, kuna baadhi ya wagonjwa wa TB waliokumbwa na wasiwasi wa unyanyapaa, vile vile maradhi ya kifua kikuu kudhaniwa kuwa Covid-19, huku wengine wakihofia kutengwa au kulazwa hospitalini.

Caroline Kathure, 52, ni mmoja wao. Yeye ni mkazi wa eneo la Chogoria, Kaunti ya Tharaka Nithi. Aligundulika kuugua TB Februari 2020.

Bi Caroline Kathure. Picha/ Pauline Ongaji

“Mwanzoni, sikujua kwamba nilikuwa na maradhi hayo kwani sikuonyesha dalili. Kwa mfano, sikuwa nakohoa,” aeleza.

Lakini kama ada, baada ya kugundulika kuugua maradhi haya, Kathure alianzishiwa matibabu, ambayo yalitarajiwa kuendelea kwa muda wa miezi sita.

“Nilienda hospitalini na kupokea matibabu yangu, ambapo nilifuata masharti vilivyo,” asema.

Lakini mambo yalibadilika ghafla mwezi Machi, baada ya mkurupuko wa virusi vya corona kutangazwa kuwa dharura ya kiafya hapa nchini Kenya, hatua iliyoambatana na marufuku ya usafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Hali ngumu ya kiuchumi ilimkabili Kathure, ambapo alilazimika kufunga duka lake la mboga mjini Chogoria. Kabla ya Covid-19 alikuwa akipata dawa zake za TB na huduma katika hospitali ya Chuka General, takriban kilomita 20 kutoka nyumbani kwake.

“Nilifanya uamuzi wa kutochukua dawa karibu na nyumbani kwangu kutokana na unyanyapaa. Nilikuwa nahofia kwamba endapo ningeonekana na mtu au watu wanaonifahamu nikipokea dawa hizi, basi wangenitenga,” aeleza.

Nauli ilikuwa Sh200, lakini alimudu kwa sababu biashara yake ilikuwa inanawiri.

Hata hivyo, hali ngumu ya kiuchumi iliyofuatana na marufuku ilimlazimu kufunga biashara yake. Aidha, pia kutokana na athari za Covid-19, gharama ya usafiri iliongezeka maradufu, na hivyo kufanya iwe vigumu hata zaidi kusafiri hadi hospitalini.

Akasalia na uamuzi wa kuchukua dawa zake katika kituo chochote cha kiafya cha serikali eneo la Chogoria, lakini kutokana na unyanyapaa aliokuwa akihofia, alilazimika kususia matibabu.

Aliacha kutumia dawa za TB kwa miezi miwili, kabla ya kurejea mwezi Juni, wakati ambapo masharti ya udhibiti wa Covid-19 kidogo yalikuwa yamelegezwa.

“Niliporejea niliwekwa katika matibabu ya miezi minane, lakini nililazimika kuanza tena. Kwa sasa nimesalia na mwezi mmoja kabla ya kukamilisha matibabu,” aongeza.

Kulingana na Pamela Njeru, mwanaharakati dhidi ya maradhi ya TB katika Kaunti ya Tharaka Nithi, huu tu ni mfano wa jinsi waathiriwa wa maradhi haya walivyoteseka katika eneo hili kutokana na athari za Covid-19.

Bi Pamela Njeru. Picha/ Pauline Ongaji

“Unyanyapaa ulichangia pakubwa tatizo la kukatiza matibabu kwa sababu kwa kawaida, wagonjwa wengi hupokea matibabu mbali na wanakoishi,” aongeza.

Kwa John Mutua, 65, kutoka eneo la Kitheini, Kaunti ya Makueni, ambaye pia matibabu yake ya kifua kikuu yalikatizwa kutokana na athari za Covid-19, hali ilikuwa tofauti kidogo. Aligundulika kuugua maradhi ya kifua kikuu Januari 2020, lakini miezi minne tu baada ya kuanza kupokea matibabu, alitoweka.

Bw John Mutua. Picha/ Pauline Ongaji

“Huo ulikuwa mwezi wa Mei mwaka jana, wakati ambapo maradhi ya Covid-19 yalikuwa yamechacha. Katika sehemu zingine za kaunti yetu, tulisikia hadithi za watu waliopelekwa katika vituo vya kutenga wagonjwa wa Covid 19, baada ya kupatikana wakikohoa. Hii kama mojawapo ya ishara za TB, singeweza hatarisha usalama wangu kwa kwenda hospitalini. Aidha, nilihofia kuambukizwa maradhi ya Covid-19,” alisema.

Mzee Mutua alitoweka kwa takriban mwaka mmoja, hadi Februari 2021, aliporejeshwa kwa matibabu.

“Wakati huo, alikuwa amedhoofika sana ambapo tulilazimkika kumbeba hadi hospitalini,” aongeza Stanslaus Mulatia, mwanaharakati dhidi ya TB na mhudumu wa kiafya wa kujitolea kutoka eneo la Wote, Kaunti ya Makueni.

Simulizi za Kathure na mzee Mutua zinatofautiana, lakini la wazi ni kwamba mkurupuko wa maradhi ya Covid-19 ulikatiza pakubwa matibabu yao, athari ambazo huenda zingeishia kuwa janga, huku mojawapo ya majanga makuu yakiwa kukumbwa na TB sugu (DRTB).

Keneti Nthitu, 40, kutoka eneo la Tononoka, kaunti ndogo ya Mvita, Kaunti ya Mombasa anajongea takwimu hiyo pia. Kulingana naye, alianza kukohoa mapema mwaka 2020.

Bw Keneti Nthitu. Picha/ Pauline Ongaji

Alienda katika hospitali tofauti eneo hilo katika harakati za kupimwa, lakini maradhi hayo hayakutambuliwa.

“Kwanza kabisa kufikia huduma hospitalini ilikuwa changamoto, sababu ikiwa kwamba kwanza niliogopa kuambukizwa maradhi virusi vya corona,” asema Nthitu.

Anne Nyambura, mwanaharakati wa maradhi ya kifua kikuu katika Kaunti ya Mombasa asema hospitali zilikuwa zinajaribu kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi ya Covid-19, huku sehemu zingine za kutoa huduma za matibabu zikibadilishwa na kuwa vituo vya Covid-19.

“Wakati huo pia, ndipo madaktari walikuwa wamegoma kulalamikia mazingira ya utendakazi hospitalini, kutokana na athari za Covid-19,” aongeza.

Nthitu alipopimwa mwezi Mei, aligundulika kuugua TB sugu.

“Mara moja niliwekwa kwenye matibabu ya miezi 18 ambapo nililazimika kuanza upya matibabu,” aliongeza.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO, kukatizwa kwa matibabu ya kifua kikuu hasa kutokana na athari za Covid-19, kumerejesha nyuma maafikio ya vita dhidi ya TB. Takwimu zilizokusanywa na WHO kutoka mataifa 84, zinaonyesha kwamba kulikuwa na upungufu wa takriban watu milioni 1.4, waliopokea matibabu ya TB mwaka wa 2020, ikilinganishwa na 2019. Upungufu huu ni wa 21%. Katika kikundi cha mataifa 10 yenye mzigo mkubwa wa TB, upungufu huu ulikuwa 28%.

Lakini japo wataalamu wanahoji kwamba ni mapema kufikia uamuzi kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa visa vya TB sugu miongoni mwa wagonjwa wanaougua kifua kikuu, kutokana na tatizo la kukatizwa kwa matibabu miongoni mwa baadhi ya wagonjwa hawa, uwezekano huu hauwezi puuzwa.

Kulingana na Wizara ya Afya, mwaka wa 2020 kulikuwa na visa 962 vya TB sugu inayokinzana na dawa kadhaa (MDR-TB), ikilinganishwa na 692, idadi ya wagonjwa wa aina hii ya TB waliopokea matibabu mwaka wa 2019, angaa kuambatana na WHO. Hilo ni ongezeko la 39%.

“Viwango vya chini vya utambuzi wa TB, wahudumu wanaoshughulikia wagonjwa wa TB kuelekezwa katika sehemu zingine, kutozingatia masharti ya matibabu kutokana na hofu ya kuambukizwa maradhi ya TB, na vituo vya matibabu ya TB kubadilishwa na kuwa wodi za Covid-19. Huenda haya yote yakawa na athari mbaya katikka ubora wa huduma ya matibabu ya TB sugu,” asema Dkt George Oballa, Mshauri wa kiufundi – Idara ya udhibiti wa TB sugu, Mpango wa Kitaifa wa TB katika Wizara ya Afya.

Kulingana na Dkt Oballa, kuna njia tatu zinazoweza kumsababisha mtu kukumbwa na TB sugu: Viwango duni vya dawa, masuala yanayohusiana na huduma ya afya, kama vile kukosa kushughulikiwa kwa wagonjwa wa TB, na hasa, masuala yanayohusiana na mgonjwa kama vile kukosa kufuatilia au kukatizwa kwa matibabu ya maradhi ya TB kutokana na sababu mbalimbali (sababu hii ndio inachangia 60% ya visa vya TB sugu).

James Irungu Karanja, 43, ni mwanamume asiye na ajira wala makao katika eneo la Godown Simanzi, Kaunti ya Mombasa. Katika kipindi cha miaka kumi, Karanja alikumbwa TB mara mbili, akapokea matibabu na kupona. Lakini Septemba 2020, alipatikana kuugua maradhi ya TB sugu.

Alirejeshwa kwa matibabu ambayo amekuwa akipokea sasa kwa miezi saba.

Lakini tatizo ni kwamba anakumbwa na hatari ya kutoendelea na matibabu kutokana na ukosefu wa chakula.

“Nilipokea mara moja tu Sh7,500, pesa zinazotolea na serikali kwa wagonjwa wa TB ili kukidhi mahitaji. Mimi humeza tembe nane kila siku, na siwezi kuendelea kutumia dawa hizi bila chakula kwani mwili wangu hauwezi stahimili,” asema.

Je, kusitisha kwake kwa matumizi ya dawa kutamaanisha nini sio tu kwa matibabu yake, bali pia kwa wenzake wasio na makao anaojumuika nao mitaani?

“Kukosa kutumia dawa za kutibu TB sugu huenda kukasababisha mgonjwa kukumbwa na aina sugu zaidi ya TB (extensively drug-resistant XDR-TB) ambayo ni ngumu kutibu kwa kutumia dawa za TB sugu,” aeleza Dkt Oballa.

Hii pia yaweza maanisha kwamba ikiwa mgonjwa atarejelea matibabu, atalazimika kuanza kumeza dawa upya, na hii pia ina hatari zake.

Ni suala ambalo Nicholas Maghanga, 44, kutoka eneo la Salaita, Kaunti ya Taita Taveta, alikumbana nalo.

Bw Nicholas Maghanga. Picha/ Pauline Ongaji

Maghanga alitambulika kuugua maradhi ya TB kwanza miaka michache iliyopita, ambapo kama ada aliwekwa kwa matibabu ya miezi sita.

Hata hivyo, baada ya matukio kadha wa kadha yaliyomsababisha kukatiza matibabu yake, maradhi haya yalichipuka mara mbili, kabla ya hatimaye kugundulika kuugua TB sugu.

Kufikia sasa amekuwa akipokea matibabu kwa miezi 15 ambapo anatarajiwa kukamilisha matibabu mwezi Juni.

Hata hivyo, kukatizwa kwa matibabu yake mara kadhaa kumemsababishia hasara kubwa. Kwanza, aliambukiza jamaa zake watatu. Pia, kulingana naye, matumizi ya dawa hizi yameathiri uwezo wake wa kusikia.

“Siwezi kusikia vyema kupitia sikio langu la kulia. Lazima uzungumze kwa sauti ya juu ili nisikie unachosema,” aongeza.

Japo hakuna ushahidi kwamba tatizo analokumbana nalo ni kutokana na matumizi ya dawa za kutibu TB sugu, kulingana na Dkt Oballa kuna athari za kiafya zinazohusishwa na matumizi ya dawa za TB sugu.

“Hatari za kiafya zaweza kuwa chache, wastani au kali kiasi cha kuwa tishio kwa maisha. Baadhi ya athari hizi ni uharibifu wa ogani muhimu mwilini hasa ikiwa matibabu hayatafuatiliwa,” aongeza.

Aidha, asema, wagonjwa hawa wanaweza kusambaza maradhi haya. Hii ina athari zaidi kwa mfumo wa afya, hasa ikizingatiwa kwamba gharama ya matibabu ya maradhi haya ni ghali mno.

Shirika la WHO linakadiriwa kwamba gharama ya matibabu ya TB sugu ni takriban US$4500, ikijumuisha pia uwezekano wa mgonjwa kulazwa kwa muda wa miezi sita.

Ili kukabiliana na tatizo hili, Dkt Oballa asema kwamba matibabu ya TB sugu sharti yafuatiliwe kwa karibu katika viwango vyote vya utawala.

Dkt Oballa, aidha anasema kwamba Wizara ya Afya kupitia washirika wa kimataifa katika vita dhidi ya TB, imepokea vifaa vya kutambua TB (GXP diagnostic) katika hospitali zote za kaunti na kadhaa za rufaa.

“Hii imenuiwa kufanya iwe rahisi kufuatilia visa vya TB sugu, vile vile kusaidia shughuli ya utambuzi wa TB sugu iwe thabiti.”

Hatua zingine ambazo serikali imechukua, asema, ni pamoja na kutumia vyombo vya habari na taasisi zingine kuhamasisha watu kuhusiana na maradhi ya TB, vile vile kupima kwa wingi jamii za wafugaji wanaohama hama.

“Na kwa mwongozo wa WHO, wataalam katika mpango wa kitaifa wa udhibiti wa TB sugu, wamekagua upya, kuunda na kusambaza miongozo mipya kuhusiana na TB sugu nchini,” aongeza.

Makala haya yameandikwa kama sehemu ya mpango wa ukuzaji ujuzi wa uanahabari, mafunzo yaliyotolewa na Hazina ya Thomson Reuters Foundation. Yaliyomo ni wajibu wa mwandishi na mchapishaji pekee.

You can share this post!

Johana na timu yake ya Jonkopings waangukia pua ligini...

‘Usilaze damu mwanamke wewe’