• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
IRENE MUKUSYA: Ninalenga kupaa anga za kimataifa kwa uigizaji

IRENE MUKUSYA: Ninalenga kupaa anga za kimataifa kwa uigizaji

Na JOHN KIMWERE

”NINATAMANI kutinga upeo wa juu katika tasnia ya maigizo.” Haya ni matamshi yake Irene Ndangwa Mukusya anayefunguka kuwa Kenya inazidi kupiga hatua katika uigizaji.

Chipukizi huyu aliyeanza kujituma katika masuala ya maigizo miaka miwili iliyopita anasema ingawa hajaiva amepania kuwa miongoni mwa wenzake watakaobadilisha sekta ya uigizaji nchini na kuifikisha ngazi ya kimataifa.

”Ninaamini kujituma na ushirikiano wetu kama wanamaigizo nchini kutasaidia pakubwa kupaisha tasnia ya uigizaji nchini,” alisema na kuongeza kuwa uhaba wa ajira umechangia wengi wao kujiunga na jukwaa hilo. Andokeza kuwa alivutiwa zaidi na uigizaji baada ya kutazama, msanii Yasmin Said maarufu Maria mhusika mkuu katika kipindi cha Maria kilichokuwa kinapeperushwa kupitia Citizen TV. Kipindi hicho kilichoanza kuonyeshwa mwaka 2019 na kusitisha mapema mwaka huu kilijizolea wafuasi wengi nchini.

JENNIFER LAWRENCE

Chipukizi huyu anayepania kufuata nyayo za mwigizaji wa kimataifa mzawa wa Marekani, Jennifer Lawrence anajivunia kushiriki filamu kadhaa tangia ajiunge na tasnia ya uigizaji. Kisura huyu aliyezaliwa mwaka 1998 anasema katika kazi zake mwigizaji huyo anapenda kutazama filamu iitwayo ‘Silver Linings Playbook.’ Kando na filamu hiyo, Jennifer ameshiriki kazi nyingi tu ikiwamo

‘American Hustle,’ ‘The hunger Games,’ na Passegers,’ kati ya zingine.

Irene anasema akifanya kazi na kundi cha M-Jey Production alifanikiwa kushiriki filamu kama ‘Tragic Valentine,’ na ‘Blood Oath.’ Pia ameshiriki ‘G-series,’ na ‘Truth or dare,’ zote Strong Pillars Entertainment.

Ndani ya miaka mitano ijayo anataka kuhakikisha kuwa anatinga hadhi ya juu na kuibuka kati ya wasanii bora wanaolipwa vyema nchini. Pia katika kipindi hicho anatamani kuorodheshwa kati ya wamiliki wa kampuni za kuzalisha filamu nchini kusudi kusaidia wasanii wanakuja kwenye gemu.

KUFANYA KAZI

Kimataifa anatamani sana kufanya kazi na waigizaji mahiri kama Lupita Nyong’o (Mkenya) kati ya wanamaigizo walioshiriki filamu ya ‘Black Panther’ na ‘Star Wars.’ Mwingine akiwa, Jackie Appiah mzawa wa Ghana aliyeigiza katika filamu kama ‘Princess Tyra,’ na ‘Heart of Men,’ kati ya zinginezo. Kwa wenzake hapa nchini anatamani kujikuta jukwaa moja nao Celestine Gachui maarufu Selina na Yasmin Said maarufu Maria.

Anasema kuwa katika masuala ya mahusiano hawezi kuweka katika kaburi la sahau kuwa aliyekuwa mpenzi wake alimtonisha chozi alipokataa kumuunga mkono jitihada zake kuwa mwigizaji.

MAWAIDHA

Anashauri wenzie wajitume mithili ya mchwa wala wasife moyo katika uigizaji kwenye jitihada za kutimiza azma yao. Anashikilia kuwa serikali inastahili kuwekeza zaidi katika sekta ya uigizaji na kuwaunga mkono wasanii wanaoibukia bila kusahau kuanzisha vituo husika katika kila Kaunti.

Anakariri kuwa kati ya changamoto ambazo amekutana nazo ni kujikuta katika kundi ambalo halina vyombo vya kufanya kazi ambapo mara nyingi hushauriwa kuchanga hela kukodisha vifaa vya kazi ilhali hawana. Anashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono kwenye juhudi za kupalilia kipaji chake katika ulingo wa burudani jambo linalomridhishia kuwa ipo siku kazi yake itakumbalika.

You can share this post!

Deby azikwa huku jeshi la nchi likigawanyika kuwili

NASAHA ZA RAMADHAN: Itambue siri kubwa ya ibada ya kufunga...