Atletico wacharaza Elche na kunusia ubingwa wa La Liga

Na MASHIRIKA

BAO la Marcos Llorente katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Atletico Madrid dhidi ya Elche lilitosha kuwadumisha kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Yannick Carrasco alishirikiana vilivyo na Llorente ndani ya kijisanduku cha Elche na kumwacha hoi kipa Paulo Gazzaniga.

Llorente alinawa mpira katika dakika ya 90 na kuwapa Elche penalti ambayo waliipoteza baada ya mkwaju wa Fidel Chaves uliomzidi ujanja kipa Jan Oblak kugonga mhimili wa goli la Atletico.

Chini ya kocha Diego Simeone, Atletico kwa sasa wamejizolea jumla ya alama 76 huku zikisalia mechi nne pekee kwa kampeni za La Liga msimu huu kutamatika rasmi.

Ni pengo la pointi mbili pekee ndilo linatamalaki kati ya Atletico na mabingwa watetezi Real Madrid walioongozwa na kocha Zinedine Zidane kuwachabanga Osasuna 2-0.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO