• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Msafara wa Suluhu wasababisha msongamano Mombasa Road

Msafara wa Suluhu wasababisha msongamano Mombasa Road

Na LEONARD ONYANGO

SHUGHULI za usafiri katika Barabara ya Mombasa – Mombasa Road – jijini Nairobi Jumanne asubuhi zilitatizika kwa saa kadhaa kufuatia msongamano mkubwa wa magari uliosababishwa na ziara ya kiongozi wa Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan humu nchini.

Baadhi ya madereva walisema kuwa walikwama barabarani kwa zaidi ya masaa manne.

Wenye magari walishutumu serikali kwa kukosa kuwatengea njia mbadala ili kuepuka msongamano kwenye barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

Baadhi ya abiria ambao hawakutaka kuchelewa kazini asubuhi walilazimika kutumia bodaboda kutoka Jumba la Kibiashara la Gatewayy hadi uwanja wa Uhuru Park ambapo walitozwa nauli ya hadi Sh1,000.

Kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), msafara wa Rais Suluhu ulipia Southern Bypass, Barabara ya Langata, Barabara ya Mbagathi hadi katika Hoteli ya Serena ambapo alipumzika kwa karibu saa moja na kisha kuelekea katika Ikulu.

Uwanjani JKIA, Rais Suluhu alilakiwa na mawaziri Raychelle Omamo (Masuala ya Kigeni), Balozi Amina Mohammed (Michezo) na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu.

Rais Suluhu pamoja na ujumbe wake waliposhuka kutoka katika ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania, Air Tanzania, saa 3.40 asubuhi, walikuwa wamevalia barakoa.

Lakini alipokuwa akiagwa na Makamu wa Rais Philip Mpango na viongozi wengine wakuu alipoondoka Tanzania, hawakuwa wamevalia barakoa.

Alipozuru Uganda, Aprili 11, mwaka huu, kiongozi huyo wa Tanzania pamoja na ujumbe wake alivalia barakoa lakini walizitoa waliporejea.

Hii ni ziara ya pili nje ya Tanzania tangu kuapishwa kuwa rais wa taifa hilo la Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Rais John Pombe Magufuli aliyeaga dunia Machi 17, 2021.

Katika Ikulu, Rais Suluhu alilakiwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kukagua gwaride la heshima na kupokea mizinga 21.

Baada ya hafla hiyo fupi, Rais Suluhu alifanya mazungumzo na Rais Kenyatta.

Kiongozi wa Tanzania anatarajia kuhutubia Bunge Jumatano saa nane na nusu mchana. Anatarajiwa kukutana na wafanyabiashara Watanzania na Wakenya na kongamano la wafanyabiashara wanawake.

Aprili 2020 Rais Kenyatta alituma waziri Amina kwenda kumwalika Rais Suluhu kuzuru Kenya – mwaliko ambao aliitikia.

You can share this post!

Ushindani wa Marekani utadhuru maslahi ya nchi za Afrika,...

Raia watatu wa kigeni watiwa mbaroni Ruiru kwa kupatikana...