• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:10 PM
KAMAU: Rais Suluhu ni mwanga halisi kuikomboa Afrika Mashariki

KAMAU: Rais Suluhu ni mwanga halisi kuikomboa Afrika Mashariki

Na WANDERI KAMAU

NI wazi kuwa Rais Samia Suluhu wa Tanzania ndiye mwanga uliohitajika kufufua tena mshikamano uliokuwa umevurugika miongoni mwa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kwa muda mfupi ambao amekuwa uongozini tangu kifo cha mtangulizi wake, Dkt John Magufuli, mnamo Machi, Rais Suluhu ameanza juhudi kabambe za kurekebisha “makosa” aliyofanya mwendazake.

Ingawa bado kuna safari ndefu inayomgoja kama rais, ameashiria kuwa kiongozi mpole, mjalifu, mpenda watu na mwenye mapenzi ya mama kwa wanawe. Ziara yake ya siku mbili nchini Kenya wiki hii bila shaka imefuta tofauti, mizozo, mivutano, taharuki na chuki zilizodhihirika wakati wa utawala wa Dkt Magufuli.

Kinyume na misimamo mikali ya kisiasa ya mtangulizi wake, Bi Suluhu ameibuka kuwa tiba inayohitajika kuziba mianya iliyokuwepo chini ya Dkt Magufuli.

Ingawa ni mwiko kuwasema vibaya wafu katika mila za Kiafrika, ucheshi na uchangamfu wa Bi Suluhu umeufanya utawala wa Dkt Magufuli kuonekana kama “kosa” lililofanyika Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla.

Japo ni kawaida kwa wanasiasa kubuni mbinu za kujipatia umaarufu miongoni mwa wafuasi wao, kosa kubwa alilofanya Dkt Magufuli ni kuingiza tofauti zake za kibinafsi katika masuala ya kidiplomasia, ambapo yaliathiri sana mahusiano ya Tanzania na majirani wake.

Chini ya utawala wa kiongozi huyo, ungedhani Wakenya na Watanzania ni maadui ambao washawahi kukabiliana kwenye vita.

Magufuli alijenga chuki na ushindani wa kisiasa usiofaa kati ya Tanzania na majirani muhimu kama Uganda, Rwanda na Burundi.

Hilo lilidhihirika hata kwenye mazishi yake, kwani kando na Rais Uhuru Kenyatta marais wote wa nchi wanachama wa EAC walikosa kuhudhuria. Badala yake, waliwatuma wawakilishi.

Hii si taswira nzuri hata kidogo, hasa kwa nchi yenye ukuaji wa kadri kama Tanzania.

Ili kutimiza malengo yake kiuchumi na kibiashara, lazima ishirikiane na majirani wake.

Misimamo mikali ya Magufuli, hasa kuhusu juhudi za kukabili virusi vya corona, pia iliwafanya baadhi ya Watanzania kutoamini janga hilo lipo duniani.

Huu ulikuwa upotoshaji mkuu na njia isiyofaa kabisa kwa kiongozi kujizolea umaarufu miongoni mwa raia.

Imani yetu ni kwamba akiwa makamu wake, Rais Suluhu aliona mapungufu hayo yote na jinsi yalivyomwathiri kila mmoja katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Tunamtakia kila la heri anapoendeleza juhudi za kurejesha urafiki na ushirikiano uliofutika chini ya utawala wa Magufuli.

[email protected]

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Mambo kwa ‘ground’ si mzaha, Wakenya...

Mombasa yatoa kanuni za sherehe za Idd kuzuia maambukizi