• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
ODM iko imara, tayari kutwaa urais – Sifuna

ODM iko imara, tayari kutwaa urais – Sifuna

Na BRIAN OJAMAA

KATIBU Mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Edwin Sifuna ameshikilia kuwa chama hicho kiko imara na kinalenga kutoa rais wa Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Sifuna alisema chama hicho kinashabikiwa kote nchini na kina wafuasi katika pembe zote za nchi.

Alisema haya wakati ambapo mgawanyiko umeibuka katika chama hicho kuhusu suala la iwapo Mswada wa BBI unapaswa kufanyiwa mageuzi au la.

Kiongozi wa wachache katika Seneti James Orengo na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo wamependekeza kuwa mswada huo ufanyiwe mageuzi.

Bw Sifuna alisema ODM inalenga kuwawezesha vijana kupata ajira, kuondoa umasikini, kufufua uchumi kati ya mipango mingine ya kuwafaa wananchi wa kawaida.

“Chama cha ODM kiko imara chini ya uongozi bora wa waziri mkuu wa zamani Raila Odinga na miye Katibu Mkuu. Kwa hivyo, nakerwa ninaposikia watu wengine ambao sio wanachama wa ODM wakieneza uvumi kwamba ODM imegawanyika kuhusiana na BBI. Eti Sifuna amepokonywa wadhifa wa Katiba Mkuu, na porojo nyingine ambazo hazina msingi wowote,” akasema.

Sifuna alisema kama Katibu Mkuu hatawavumilia watu wenye nia ya kuvuruga chama cha ODM kwa malengo yao ya kibinafsi.

“Ikumbukwe kwamba nilipochukua hatamu kama Katibu Mkuu, nilibainisha wazi kwamba sitaruhusu chama hiki kudunishwa na marafiki zetu katika muungano wa NASA. Wasidhani kuwa tuko sawa na wao; ODM iko mbele kabisa,” akasema.

Bw Sifuna aliwataka wanachama wa ODM kutotishika wala kuingiwa na wasiwasi wanaposikia kelele na propaganda kutoka kwa marafiki zao katika NASA ambao walitengana nao zamani kwa kutofautiana.

“Nitaendelea kutekeleza wajibu wangu kama Katibu Mkuu kwa moyo wangu wote na bila woga. Na sitarajii washindani wetu kufurahia kazi zangu,” akasema.

“Kama chama tulitangaza kuwa baada ya Mswada wa BBI kupita katika kura ya maamuzi, tutaweka mikakati ya kuanza safari ya kuelekea Ikulu na kuunda serikali ijayo. Tutafanya hivyo kwa kushirikiana na marafiki zetu tunaowaamini na kuwa na maoni sawa nao,” akaelezea.

Bw Sifuna alisema kwa wakati huu haja kubwa ya ODM ni kuhakikisha kuwa Mswada wa BBI umepita ili kuifanya Kenya kuwa nchini nzuri.

“Baada ya hapo tutaanza harakati za kubuni miungano kwa ajili ya kuunda serikali ijayo. Hatutaungana na vyama ambavyo vitaishia kuwa mzigo kwetu tulivyofanya miaka ya nyuma.

“Kwa mfano, ukiuliza wafuasi wa ODM hapa Bungoma, watasema wazi kuwa miungano ya CORD na NASA ilichangia chama chetu kupoteza viti kule mashinani katika changuzi za 2013 na 2017, ikiwemo hapa Bungoma,” Bw Sifuna akasema.

Alisema akiwa Katibu Mkuu atahakikisha kuwa ODM inashinda viti vya ugavana, useneta, ubunge na udiwani katika kaunti ya Bungoma wakati wa uchaguzi mkuu ujao mwaka wa 2022.

Mapema wiki hii Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alionya kuwa Mswada wa BBI unaweza kusambaratisha chama hicho. Hata hivyo, wabunge wa chama hicho waliuunga ulipopigiwa kura bungeni

You can share this post!

Solskjaer alia ugumu wa ratiba ya Man-United watakaopiga...

Kampuni ya Mumias mbioni kurejelea usagaji wa miwa