• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Mashambulio yatokea Afghanistan kipindi Amerika iko mbioni kuondoa wanajeshi wake

Mashambulio yatokea Afghanistan kipindi Amerika iko mbioni kuondoa wanajeshi wake

Na AFP

KABUL, Afghanistan

WATU zaidi ya 20 wameuawa na wengine 52 wakajeruhiwa katika mlipuko uliotokea Jumamosi nje ya shule moja jijini Kabul, Afghanistan, Wizara ya Masuala ya Ndani imesema.

“Inasikitisha kuwa watu 26 wameuawa na 52, wakiwemo watoto wamejeruhiwa na kupelekwa katika hospitali mbalimbali,” msemaji wa wizara hiyo Tareq Arian aliwaambia wanahabari huku akionya kuwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka.

Mlipuko huo ulitokea magharibi mwa Kabul katika kitongoji cha Dasht-e-Barchi wakati wakazi walikuwa wakiendesha shughuli za kununua mahitaji mbalimbali kwa sherehe za Idd-ul-Fitr juma lijalo. Siku kuu hiyo ndio huashiria mwisho wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ambapo Waislamu kote ulimwenguni hufunga.

Watu wa kabila la Shia Hazaras ndio huishi kwa wingi katika kitongoji hicho na hulengwa kila mara na baadhi ya wenye kuegemea Sunni.

Naibu Msemaji wa Wizara hiyo ya Masuala ya Ndani Hamid Roshan aliambia shirika la habari la AFP kwamba uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini cha shambulio hilo. Hata hivyo, alisema alisema hilo lilikuwa shambulio la kigaidi.

Msemaji wa Wizara ya Afya Dastagir Nazari alisema ambulensi kadha zilifika katika eneo la tukio na kuwakimbiza hospitalini.

“Watu katika eneo hilo wamejawa na hasira na wamewachapa wafanyakazi wa ambulensi,” aliwaambia wanahabari.

Shambulio hilo lilitokea wakati ambapo Amerika ilikuwa ikiendelea na shughuli ya kuwaondoa kundi la mwisho la wanajeshi wake 2,500 kutoka Afghanistan.

Hii ni licha ya kuwepo kwa hofu ya kusambaratika kwa juhudi za kupalilia amani kati ya kundi la Taliban na Serikali na hivyo kukomesha vita vilivyodumu miongoni kadhaa nchini Afghanistan.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Lille wakomoa Lens na kuweka mkono mmoja kwenye taji la...

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya afisa wa NLC anyakwa