• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Manchester City kusubiri zaidi kutwaa taji la EPL baada ya kupigwa 2-1 na Chelsea

Manchester City kusubiri zaidi kutwaa taji la EPL baada ya kupigwa 2-1 na Chelsea

Na MASHIRIKA

SERGIO Aguero alipoteza penalti katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ulioshuhudia Chelsea wakiwapokeza kichapo cha 2-1 mnamo Jumamosi ugani Etihad.

Matokeo hayo yaliwasaza Man-City katika ulazima wa kusubiri zaidi kabla ya kutawazwa mabingwa wa taji la EPL muhula huu na kwa mara ya saba.

Man-City walioingia ugani wakihitaji alama tatu pekee ili kutwaa ufalme wa muhula huu, waliwekwa kifua mbele na Raheem Sterling mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, walipoteza fursa ya kufanya mambo kuwa 2-0 mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya Aguero kupoteza penalti iliyotokana na tukio la Gabriel Jesus kuchezewa visivyo na Billy Gilmour ndani ya kijisanduku. Mkwaju huo wa Aguero atakayeagana rasmi na Man-City mwishoni mwa msimu huu, ulidhibitiwa vilivyo na kipa Edouard Mendy wa Chelsea.

Aguero alijutia pakubwa kupoteza penalti hiyo kwa kuwa tukio hilo liliwapa Chelsea motisha ya kurejea mchezoni kwa matao ya juu na wakasawazishiwa na Hakim Ziyech katika dakika ya 63 kabla ya Marcus Alonso kushirikiana na Timo Werner na kufunga goli la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ushindi huo ulikuwa wa pili kwa Chelsea kusajili dhidi ya Man-City chini ya kipindi cha wiki tatu baada ya kuwadengua kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA ugan Wembley, Uingereza mnamo Aprili.

Vikosi hivyo viwili vitakutana tena kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 29 jijini Istanbul, Uturuki.

Ni matarajio ya kocha Thomas Tuchel wa Chelsea kwamba ushindi mara mbili dhidi ya Man-City utawapa masogora wake motisha zaidi ya kuvuna ushindi mwingine wa tatu dhidi ya miamba hao wa EPL na kutia kapuni taji la UEFA hatimaye.

Kocha Pep Guardiola alikifanyia mabadiliko kikosi chake cha Man-City kilichodengua Paris Saint-Germain (PSG) kwenye nusu-fainali ya UEFA mnamo Jumanne iliyopita mabadiliko tisa huku Tuchel akifanyia kikosi alichokitegemea dhidi ya Real Madrid kwenye mkondo wa pili wa nusu-fainali ya UEFA mabadiliko matano.

Mamia ya mashabiki waliokuwa wamekongamana nje ya uwanja wa Etihad tayari kusherehekea ushindi wa Man-City walivunjwa moyo na matokeo ya kikosi chao kinachosubiri kutawazwa wafalme wa EPL kwa mara ya tatu chini ya kipindi cha misimu minne iliyopita.

Hata hivyo, huenda Man-City wakatwaa taji la EPL msimu huu kabla ya kupiga mechi yao ijayo dhidi ya Newcastle United mnamo Ijumaa iwapo Manchester United watapoteza alama muhimu katika mechi tatu zijazo watakazopiga ligini chini ya kipindi cha siku tano. Hata hivyo, ushindi kwa Man-United katika michuano hiyo utapunguza uongozi wa Man-City kileleni mwa jedwali hadi alama nne pekee.

Japo alitarajiwa kufanya mabadiliko baada ya mechi dhidi ya PSG, Guardiola alilaumiwa kwa maamuzi ya kubadilisha hata mfumo wa mchezo kutoka ule wa 4-3-3 ambao wametegemea sana muhula huu hadi 5-1-3-1 ambao wanasoka wake hawajazoea.

Chelsea kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 64, tatu nyuma ya Man-United ambao wana mechi tatu zaidi za kutandaza ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na masogora wa Tuchel. Leicester wanajivunia pointi 63 huku pengo la alama 17 likiwatenganisha na viongozi Man-City.

Chelsea kwa sasa wanajiandaa kuwa wenyeji wa Arsenal ligini mnamo Jumatano ya Mei 12, siku mbili kabla ya Man-City kuwaendea Newcastle ugani St James’ Park.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Bayern Munich watia kapuni taji la Bundesliga kwa mara ya...

Huenda Clarke Oduor akajiengua Barnsley iliyomfanya shabiki...