• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Huenda Clarke Oduor akajiengua Barnsley iliyomfanya shabiki mechi 27 zilizopita

Huenda Clarke Oduor akajiengua Barnsley iliyomfanya shabiki mechi 27 zilizopita

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Clarke Oduor anahusishwa na kuondoka Barnsley katika kipindi kirefu cha uhamisho kitakachofunguka Julai 1.

Barnsley inashiriki Ligi ya Daraja ya Pili Uingereza ambayo imekamilika Mei 8. Timu hiyo imetoka 2-2 dhidi ya viongozi Norwich na kukamilisha msimu wa kawaida katika nafasi ya tano. Itamenyana na Swansea katika nusu-fainali ya kutafuta timu ya tatu itakayoshiriki Ligi Kuu msimu 2021-2022. Nusu-fainali nyingine ni kati ya Brentford na Bournemouth. Zitasakatwa Mei 17 na Mei 22. Norwich na Watford walinyakua tiketi za moja kwa moja kuingia Ligi Kuu baada ya kukamilisha ligi ya daraja ya pili katika nafasi mbili za kwanza. Brentford, Swansea, Barnsley na Bournemouth zilimaliza katika nafasi ya tatu hadi sita, mtawalia.

Beki huyo, ambaye alisaidia Barnsley kukwepa kushushwa hadi daraja ya tatu msimu 2019-2020, hajatumiwa katika michuano 27 zilizopita ligini. Kocha mpya Mfaransa Valerien Ismael amemweka kitini katika mechi hizo zote pamoja na mbili kwenye Kombe la FA.

Mara ya mwisho Oduor alichezea Barnsley ni Desemba 19 mwaka jana wakati timu hiyo ilipoteza 2-0 dhidi ya Swansea.

Amesakata michuano 13 katika mashindano yote msimu huu, akikosa tatu akiwa na jeraha la kinena kati ya Desemba 12 na Desemba 19 mwaka 2020.

Oduor alifunga bao la ushindi dakika ya mwisho Barnsley ikiduwaza Brentford 2-1 Julai 22 mwaka jana timu hiyo ikikwepa kuangukiwa na shoka ikiwa chini ya kocha Gerhard Struber.

Mchezaji huyo, ambaye atagonga umri wa miaka 22 mnamo Juni 25, anahitaji kupata timu itakayomtumia zaidi ili afufue soka yake.

Mzawa huyo wa kaunti ya Siaya, ambaye ana uraia wa Uingereza pia baada ya familia yake kuhamia humo, amechezea timu ya taifa ya Kenya mara moja. Alishiriki mechi ya kirafiki dhidi ya Chipolopolo ya Zambia ambayo Harambee Stars ilishinda 2-1 Oktoba 9 mwaka jana jijini Nairobi.

You can share this post!

Manchester City kusubiri zaidi kutwaa taji la EPL baada ya...

Papa Francis aunga kuondolewa kwa ulinzi wa hakimiliki za...