• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Waombaji wasiotenda

Waombaji wasiotenda

Na BENSON MATHEKA

VIONGOZI wa kisiasa nchini jana walishutumiwa vikali wakati wa maombi ya kitaifa, kwa kuendelea kuonyesha unafiki mkubwa machoni mwa Wakenya.

“Tuache unafiki. Imani na matumaini peke yake hazitaweza kutusaidia. Tunahitaji vitendo. Kwa hivyo tukitoka hapa, twende tuchukue hatua,” akasema Seneta Amos Wako wa Busia kwenye hafla iliyohudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto katika Majengo ya Bunge.

Bw Wako alisema inasikitisha kuwa Wakenya wengi hawawezi kumudu gharama ya matibabu yakiwemo ya Covid 19, licha ya ahadi nyingi za serikali ya Jubilee za kutekeleza mpango wa Afya kwa Wote.

Wakili Peter Waiyaki, ambaye alikuwa mnenaji rasmi kwenye hafla hiyo, alisema Wakenya wanaweza kupata matumaini ya dhati wakipalilia uadilifu katika uongozi, kukumbatia uzalendo, kutekeleza na kuonyesha kwa vitendo kwamba wamejitolea kufanya hivyo.

“Uadilifu ni kutimiza unayoahidi kufanya. Kukosa uadilifu kunawapokonya raia matumaini na kuharibu nchi,” akasema Bw Waiyaki.

Wakili huyo alisema viongozi hawafai kutarajia Wakenya kuwa waadilifu ikiwa wao wanapuuza maadili na utawala wa kisheria.

“Ni jukumu la kila mtu kuwa muadilifu. Ikiwa hauwezi kuzingatia na kudumisha uadilifu, jiuzulu wadhifa wako,” akasisitiza Bw Waiyaki.

Bw Waiyaki alisema kama viongozi wa Kenya wangekuwa wazalendo, hakungekuwa na uporaji wa mali ya umma na kudhulimiwa kwa wananchi.

Jumbe za Bw Wako na Bw Waiyaki ziliwalenga viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakitenda kinyume na matamshi yao.

Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta aliwataka viongozi kuwajibika zaidi kwa vitendo vyao badala ya kuzungumza mazuri kwenye mkutano kama wa jana na kueneza migawanyiko baadaye.

“Tumesikia yaliyohimizwa hapa na siwezi kuondoa hata moja. Tungekuwa watu wa vitendo, maadili, uwajibikaji na kutenda haki, nchi ingekuwa na matumaini,” akasema.

Rais Kenyatta mwenyewe amekuwa na mazoea ya kukiuka maagizo ya mahakama na kutotimiza ahadi zake kwa umma hasa Ajenda Nne Kuu za afya kwa wote, nyumba za bei nafuu, viwanda na utoshelevu wa chakula.

Hapo jana alilaumu bunge kwa kuchelewesha sheria za kufanikisha ajenda zake hasa kuhusu utekelezaji wa afya kwa wote. Hii ni licha ya ukweli kuwa mpango huo ulikwama katika awamu ya majaribio katika baadhi ya kaunti.

Katika mikutano ya awali ya maombi, wanasiasa hao wakiwemo Rais Kenyatta, Dkt Ruto, Raila Odinga (ODM) na Kalonzo Musyoka (Wiper) wamekuwa wakiahidi makubwa, lakini muda mfupi baadaye huwa wanapuuza ahadi zao.

Hapo jana, viongozi hao wa kisiasa walinukuu maandiko matakatifu na kuomba huku wakitoa jumbe za matumaini kwa Wakenya, ambazo ni kinyume na vitendo vyao.

Walieleza matumaini ya Kenya kushinda janga la corona, ingawa waliodaiwa kupora mabilioni yaliyotengwa kukabili ugonjwa huo hawajachukuliwa hatua hata baada ya Rais Kenyatta kutoa agizo hilo mwaka jana. Baadhi ya waliotajwa katika sakata hiyo ni washirika wa viongozi wakuu serikalini.

Maombi hayo yalifanyika wakati kuna mgawanyiko mkubwa katika serikali na nchi kutokana na tofauti kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto hasa kuhusu siasa za urithi na mchakato wa BBI.

Ingawa viongozi wa kisiasa, kidini na sekta ya kibinafsi waliozungumza walisema kwamba ni muhimu kuungana kukabili changamoto zinazoikumba nchi, tofauti za rais na naibu wake zilikuwa wazi hata katika mkutano huo wa jana.

Dkt Ruto amekuwa akikosekana katika hafla za Rais Kenyatta ukiwemo ufunguzi wa Bandari ya Lamu, ambao alitaja jana kama mojawapo wa mambo mazuri yanayoleta matumaini nchini.

You can share this post!

Wapingao BBI wataka rufaa isikizwe na majaji 11

Aliyejeruhiwa akivuka feri Likoni kulipwa Sh418,000