• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Hedhi salama bado ni changamoto kwa wasichana shuleni

Hedhi salama bado ni changamoto kwa wasichana shuleni

Na PAULINE ONGAJI
UKOSEFU wa misala au vyoo safi shuleni kunachangia katika kudorora kwa masomo miongoni mwa wasichana kote nchini.

Karibu asilimia 90 ya vyoo katika shule za msingi na sekondari humu nchini havijatimiza viwango vinavyopendekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto (Unicef) ili kuwezesha wanafunzi wa kike kudumisha usafi wakati wa hedhi.

Uchunguzi uliofanywa na jarida la Afya na Jamii wakati wa maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani Ijumaa iliyopita, ulibaini kuwa shule nyingi nchini zina vyoo vibovu vinavyosababisha wasichana kutoweka shuleni wakati wa hedhi.Siku ya Hedhi Duniani huadhimishwa Mei 28 kila mwaka.

Hii ni kwa sababu mzunguko wa hedhi huwa siku 28 na maumivu au damu ya hedhi hutokea ndani ya siku tano.Vyoo vya shule nyingi nchini, haswa za umma, hazina milango, ni vichafu na havina umeme au mwangaza ndani.

Katika Shule ya Msingi ya Makutano, mjini Kapenguria, Kaunti ya Pokot Magharibi, kwa mfano, vyoo vya wasichana vimechakaa, havina milango na hivitoshi.Katika shule ya msingi jirani ya Lopelekwa, hali ni sawa na hiyo – ndani ni giza totoro milango inapofungwa hivyo ni vigumu kwa wanafunzi wa kike kufanya usafi wakati wa hedhi.

Katika Shule ya Upili ya Mnagei ambapo karibu asilimia 95 ya wasichana wanapata hedhi, vyoo pia ni vibovu na vimetengenezwa kwa mabati.Vyoo vya shule nyingi zilizoko katika mitaa ya mabanda jijini Nairobi pia vimechakaa na havijakaribia hata kutimiza asilimia 50 ya vigezo vilivyowekwa na Unicef.

Kulingana na mwongozo wa Unicef, bafu au vyoo vya wasichana shuleni vinafaa kuwa vingi kuliko vya wavulana.“Hii ni kwa sababu wasichana huchukua muda mrefu msalani ikilinganishwa na wavulana,” unasema mwongozo wa Unicef.

“Wanafunzi wa kike wanapokuwa shuleni, kuna uwezekano kwamba asilimia 20 kati yao wako katika kipindi cha hedhi na wanapoenda chooni au bafuni wanahitaji muda zaidi kufanya usafi hivyo kusababisha foleni nje,” inaongezea.Vyoo vya wasichana vinastahili kuwa na kioo ambapo wasichana watajiangalia kuhakikisha kwamba hawana matone ya damu kwenye nguo baada ya kutumia choo.

“Msichana anapokuwa na matone ya damu kwenye nguo anaweza kuchekwa au kukejeliwa na wenzake hivyo kumfanya kuhepa shuleni. Wakati ambao wanapoteza wakiwa nyumbani wakati wa hedhi unasababisha wengi wao kufanya vibaya katika masomo,” inasema Unicef.

Tafiti ambazo zimefanywa zinaonyesha kuwa wavulana au wanaume wanachukua wastani wa sekunde 60 chooni lakini wasichana au wanawake wanachukua angalau dakika 90.“Hiyo inamaanisha kuwa vyoo vya wasichana vikiwa vichache au vikiwa idadi sawa na vya wavulana, kutakuwa na msongamano wa foleni ndefu,” unasema mwongozo wa Unicef.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa kwa mfano, linapendekeza kwamba wavulana wakiwa na choo kimoja, wasichana wawe na vyoo vitatu.Unicef pia linapendekeza kuwa vyoo au bafu inayotumiwa na wasichana iwe na sabuni na maji safi.Mratibu wa shirika la Yang’at, Elizabeth Kukat, anasema kuwa wasichana wa kuanzia umri wa miaka 16 katika Kaunti ya Pokot Magharibi wanakumbwa na changamoto kubwa kufanya usafi wakati wa hedhi.“Wasichana wengi hukimbilia msalani wanapopatwa na hedhi ili kufanya usafi.

Lakini ikiwa vyoo havina milango watafanyia usafi wapi? Kuna haja ya kujenga vyoo vingi katika shule za eneo hili,”anasema.Bi Kukat anasema kuwa mazingira mabovu msalani huwafanya wanafunzi wengi kusalia nyumbani wakati wa hedhi na hili limechangia kudorora kwa elimu katika eneo hilo.

“Kusumbuka kwa mtoto wa kike wakati wa hedhi kumeweka masomo yao hatarini,” anasema.Anasema kuwa changamoto kubwa hukumba wasichana wenye ulemavu katika shule za mseto.Vyoo, maji safi na sodo

Teresa Cheptoo wa shirika la World Vision anasema kuwa licha ya juhudi nyingi za serikali, mashirika ya kijamii na watu binafsi kumsitiri mtoto wa kike na mwanamke katika jamii katika kupata hedhi ya heshima, bado kuna changamoto nyingi kwa wasichana haswa katika sehemu za nchi zilizosalia nyuma kimaendeleo kama vile maeneo ya vijijini.

“Harufu mbaya kwenye vyoo, kukosa milango na vingine kuwa na mianya hufanya wasichana wengi kuwa na wasiwasi tele,”alisema.Bi Cheptoo anasema kuwa shida nyingine kwenye shule nyingi ni uhaba wa maji kwa wasichana kujisafisha wakati wa hedhi.

“Suala la hedhi ni la siri na wasichana wanafaa kuwa na sodo za kutosha. Wengi huwa na sodo moja na wengi huzirudia mara nyingi na ni hatari kwa afya yao,” anasema.Afisa huyo wa shirika hilo lisilo la kiserikali anasema kuwa changamoto hizo kama vile ukosefu wa vyoo, maji safi shuleni na sodo zinafanya mtoto wa kike kubaguliwa wakati wa hedhi.

“Tunapata ripoti kuwa wengi wanakejeliwa na wenzao wa kiume haswa wakati wa hedhi,” anasema.Bi Cheptoo anasema kuwa mzunguko wa siku za hedhi kwa mtoto msichana katika jamii ya Pokot ni jambo ambalo huwa halizungumzwi hadharani kutokana na imani za kidini na kitamaduni.

Anasisitiza kuna haja ya wazazi kuweka bajeti ya sodo sawia na ile ya vitabu ama kalamu kwani ni hitaji maalumu kwa mtoto msichana.Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kuwa choo kimoja kitumiwe na wanafunzi wa kiume 30 au wa kike 25.

Hiyo inamaanisha kuwa shule iliyo na wanafunzi wa kike 500, kwa mfano inastahili kuwa na vyoo 20.Inakadiriwa kuwa jumla ya wasichana milioni 130 hawako shuleni kote duniani kutokana na sababu mbalimbali. Lakini kulingana na Unicef, miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha wasichana kukosa shuleni ni ukosefu wa miondomsingi ya kuwawezesha kudumisha usafi wakati wa hedhi.

Shirika hilo linakadiria kuwa msichana mmoja kati ya 10 hulazimika kukaa nyumbani wakati wa hedhi. Inakadiriwa kuwa baadhi ya wasichana hupoteza asilimia 20 ya muda wa masomo yao kutokana na hedhi. Hali hiyo husababisha baadhi ya wasichana kuachana na masomo.Mbali na vyoo vibovu, tafiti zinaonyesha kuwa karibu asilimia 60 ya wasichana hawamudu gharama ya sodo.

Naibu Gavana wa Nyeri Dkt Caroline Karugu, sasa anataka serikali kutoa sodo katika kila shule nchini ili kuwezesha wasichana kuendelea na masomo yao hata wakati wa hedhi.“Serikali imekuwa ikitoa kondomu za bure katika maeneo ya umma nchini. Vivyo hivyo, serikali inastahili kutoa sodo katika shule zote nchini,” anasema.

Utafiti uliofanywa 2016 nchini Kenya na kampuni ya FSG Consulting kwa udhamini wa Wakfu wa Bill and Melinda Gates ulibaini kuwa utamaduni na imani za kidini ni miongoni mwa changamoto kuu zinazokumba wasichana wakati wa hedhi.Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 50 ya wasichana hawawezi kujadili suala la hedhi nyumbani.

Idadi kubwa ya wasichana hawawezi kujadili suala la hedhi na mama zao.Aidha ulibaini kuwa ni asilimia 32 ya shule za vijijini zilizo na chumba maalumu cha wanafunzi wa kike kubadili sodo wakati wa hedhi.Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa idadi kubwa ya wasichana hupewa sodo na wapenzi wa kiume.

You can share this post!

Likizo ni muhimu sana kwa afya ya akili ya wanafunzi

Muthama atoa masharti makali kabla ya kuridhiana na Kalonzo