Watakaofichua sakata za ufisadi katika idara za serikali kutunukiwa Sh2 – 5 milioni kila mmoja

Na SAMMY WAWERU

WATAKAOPULIZA kipenga kuhusu sakata za ufisadi na ubadhirifu wa fedha katika idara za serikali watapata tuzo ya pesa kati ya Sh2 – 5, kila mmoja. 

Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yattani amesema hatua hiyo itasaidia kuokoa mali ya umma, yanayoendelea kufujwa na wafanyakazi na viongozi wenye tamaa. “Watakaopuliza kipenga kuhusu wizi wa fedha katika idara za serikali, tutawapa motisha kwa kuwatuza kwa kima cha kati ya Sh2 – 5, kila mmoja,” akasema Bw Yattani. 

Balozi Yattani alitoa ahadi hiyo wakati akisoma Makadirio ya Bajeti Mwaka wa Fedha 2021/2022. “Hatua hiyo itasaidia kunusuru mali ya umma, yasifujwe,” akasema Waziri Yattani, akiongeza kusema kuwa hilo pia litashirikisha wanaokwepa kulipa ushuru.

Baadhi ya viongozi katika idara mbalimbali za serikali, wamejipata kuandamwa na mkono wa sheria kufuatia tuhuma za kushiriki kashfa za ufisadi, matumizi mabaya ya mali ya umma na ofisi.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu na mwenzake wa Nairobi, Bw Mike Sonko walivuliwa mamlaka kufuatia sakata za ufisadi, ufujaji wa mali ya umma na matumizi mabaya ya ofisi.