• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Pigo tena kwa Uhuru korti ikibatilisha amri

Pigo tena kwa Uhuru korti ikibatilisha amri

Na BENSON MATHEKA

MAHAKAMA Kuu inaendelea kuwa pigo kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa kufuta maamuzi yake ikisema si ya kikatiba.

Jana, Jaji James Makau alibatilisha amri ambayo Rais Kenyatta alitoa mapema mwaka jana akiweka Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) chini ya Afisi ya Mwanasheria Mkuu.

Kwenye amri hiyo, Rais Kenyatta pia alihamisha tume huru za kikatiba kuwa chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu.Katika uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Jaji Makau alisema kwamba amri hiyo ilikiuka katiba ya Kenya na kuhatarisha uhuru wa Mahakama kwa kuwa haikufanywa kwa kuzingatia katiba.

“Imeamuliwa kwamba agizo la Rais nambari 1 la 2020 lililonuia kubadilisha serikali na kuweka mahakama na tume huru chini ya wizara na idara za serikali si la kikatiba na kwa hivyo limefutwa,” alisema Jaji Makau kwenye uamuzi wake.

Ni katika amri hiyo ambapo Rais Kenyatta aliunda Idara ya Jiji la Nairobi (NMS). Katika uamuzi mwingine mwaka jana ambao ulikuwa pigo kwa Rais Kenyatta, Mahakama Kuu iliamua kwamba kuhamishwa kwa baadhi ya majukumu ya serikali ya Kaunti ya Nairobi hadi idara hiyo, hakukuwa kwa kikatiba.

Mnamo Mei mwaka huu, mahakama Kuu iliamua kwamba uteuzi wa wakuu wa mashirika ya serikali ambao Rais Kenyatta alifanya kuanzia 2018 haukuwa wa kikatiba. Katika kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute, majaji waliamua kwamba hakukuwa na uwazi katika uteuzi huo inavyohitaji katiba.

Pia mnamo Aprili mahakama iliamua kwamba nyadhifa za mawaziri wasaidizi ambazo Rais Kenyatta alibuni ni haramu kwa kuwa hazitambuliwi katika katiba.Uamuzi huo ulijiri baada ya mwingine ambao majaji watano wa Mahakama Kuu George Odunga, Joel Ngugi, Teresia Matheka, Jairus Ngaa na Chacha Mwita, walisitisha Mswada wa kurekebisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) wakisema kwamba haukuwa wa kikatiba.

Majaji hao walisema kwamba Rais Kenyatta anaweza kushtakiwa binafsi kwa makosa yasiyohusu wadhifa wake wa kiongozi wa nchi. Rais Kenyatta ni miongoni mwa waliowasilisha rufaa dhidi ya uamuzi huo. Mapema wiki hii, serikali ilipoteza rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ulioruhusu wakili Miguna Miguna kurejea nchini.

Makabiliano ya serikali ya Jubilee na Mahakama yalianza 2017, Mahakama ya Juu ilipofuta matokeo ya uchaguzi wa urais kwa msingi kuwa haukuwa umetimiza mahitaji ya kisheria na kikatiba. Wiki jana, makabiliano hayo yaliendelea Rais Kenyatta alipokataa kuapisha majaji sita kati ya 40 walioteuliwa na JSC mwaka wa 2019.

Ilichukua Rais Kenyatta miaka miwili kuapisha majaji hao licha ya Mahakama kuamua mara mbili kwamba alikuwa amekiuka katiba kwa kukataa kuwaapisha. Mawakili wamemlaumu Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki, wakisema ameshindwa kumshauri Rais ipasavyo na kuchangia kuaibishwa kwa serikali na mahakama.

Baadhi ya mawakili wamemtaka Bw Kihara kujiuzulu wadhifa wake kwa kushindwa kumshauri ipaswavyo. Kulingana na wakili Waikwa Wanyoike, Bw Kihara na mawakili wanaohudumu chini yake hawawezi kuepuka lawama kufuatia kufutwa kwa amri ya Rais na Mahakama Kuu.

“Je, kweli kuna sifa zozote za kitaalamu zilizobaki kwa Mwanasheria Mkuu na mawakili walio chini yake,” alihoji Bw Wanyoike akirejelea msururu wa maamuzi ya Mahakama ambayo yamekuwa pigo kwa Rais Kenyatta na serikali yake

  • Tags

You can share this post!

Covid-19: Fainali za Copa America nchini Brazil kuendelea...

Afrika iongoze ukuzaji wa Kiswahili kimataifa