• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wakili wa Ruto kuapishwa wiki ijayo kumrithi Bensouda

Wakili wa Ruto kuapishwa wiki ijayo kumrithi Bensouda

Na VALENTINE OBARA

ALIYEKUWA wakili wa Naibu Rais William Ruto katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Bw Karim Khan, amepangiwa kuapishwa kuwa Mkuu wa Mashtaka wa mahakama hiyo wiki ijayo.

Bw Khan alipata wadhifa huo baada ya kupata kura nyngi za wanachama wa ICC mnamo Februari mwaka uliopita. Alimshinda wakili wa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, Bw Fergal Geynor, ambaye uwaniaji wake ulikuwa umepata pingamizi kutoka kwa serikali ya Kenya.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi usiku, mahakama hiyo ilisema hafla ya kumwapisha Bw Khan itafanyika katika makao makuu ya ICC jijini The Hague, Uholanzi. Wakili huyo Mwingereza aliye na tajriba ya juu kuhusu sheria zinazohusu uhalifu dhidi ya haki za kibinadamu kimataifa, atachukua mahali pa Bi Fatou Bensouda na kuhudumu kwa miaka tisa.

“Bw Khan atakula kiapo kutekeleza majukumu yake na mamlaka yake kama mkuu wa mashtaka wa ICC kwa uaminifu na bila mapendeleo na kuheshimu usiri wa upelelezi na uongozi wa mashtaka,” ikasema taarifa ya ICC kwa vyumba vya habari.

Hafla hiyo itaongozwa na Rais wa Baraza la Mataifa Wanachama wa ICC lililo maarufu kama ASP, Silvia Fernández de Gurmendi, na Jaji Piotr Hofma?ski, ambaye ndiye Rais wa Mahakama. Bw Khan ataingia mamlakani wakati ambapo mahakama hiyo inasubiriwa kuamua iwapo wakili Paul Gicheru atafunguliwa mashtaka kuhusu madai ya kuvuruga kesi iliyomkabili Dkt Ruto.

Awali, ICC ilitangaza kuwa Bw Khan anatarajiwa kutojihusisha na kesi zozote ambazo huenda akaonekana kuwa na mapendeleo au ubaguzi, na atazikabidhi kwa wenzake katika idara hiyo atakayosimamia.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa Bw Gicheru alikuwa katika kikundi cha watu waliopewa mamilioni ya pesa na Dkt Ruto kuhonga mashahidi waliotegemewa na Bi Bensouda, ili wabadilishe ushahidi wao dhidi yake.

Kulingana na Bi Bensouda, njama hii ilikuwa miongoni mwa sababu zilizosababisha kesi ya Dkt Ruto na mwanahabari Joshua Sang kusitishwa. Hata hivyo, Bw Gicheru amepinga madai hayo na kutaka kesi inayoandaliwa dhidi yake isikubaliwe na majaji kwa kuwa anaamini hana hatia.

Licha ya kuwa kesi za Dkt Ruto na Rais Uhuru Kenyatta zilisitishwa, mahakama ilisema upande wa mashtaka uko huru kuzifufua endapo ushahidi mpya utapatikana baadaye. ICC hutenga bajeti ya upelelezi wa kesi hizo kila mwaka.

Uamuzi huo wa majaji kutoamua kama washtakiwa wana hatia au la, ulikosolewa na jopo la wataalamu waliopewa jukumu la kutoa mwongozo wa utendakazi bora wa mahakama hiyo mwaka uliopita. Kulingana nao, hilo ni mojawapo na masuala yanayofanya ICC ionekane kama shirika linalotumiwa kisiasa kukandamiza baadhi ya mataifa ya Afrika.

  • Tags

You can share this post!

Njama ya serikali kuandaa refarenda yafichuka

Maafisa wahofia wagonjwa huiba vyandarua vya mbu