• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Copa America kung’oa nanga leo usiku

Copa America kung’oa nanga leo usiku

BRASILIA, Brazil

KIPUTE cha kuwania ufalme wa Copa America kinaanza leo usiku ugani Nacional de Brasilia kwa gozi litakalokutanisha Venzuela na mabingwa watetezi Brazil ambao pia ni wenyeji.

Katika mechi nyingine, Colombia watapimana ubabe na Ecuador jijini Cuiaba. Colombia watashuka dimbani wakipania kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 3-0 dhidi ya Peru na sare ya 2-2 dhidi ya Argentina katika mechi mbili zilizopita za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Samba Boys wa Brazil wanapigiwa upatu wa kuokota alama tatu muhimu dhidi ya Venezuela na hatimaye kuhifadhi taji la Copa America walilolinyanyua mnamo 2019 wakiwa waandalizi wa kinyang’anyiro hicho.

Brazil walipokezwa idhini ya kuwa wenyeji wa Copa America mwaka huu baada ya maandamano ya raia dhidi ya serikali kuzuka nchini Colombia na maambukizi ya virusi vya corona kuzidi nchini Argentina.Colombia na Argentina ndio waliokuwa wawe waandalizi wa pamoja wa fainali za Copa America mwaka huu na ingekuwa mara ya kwanza tangu 1916 kwa fainali hizo kuandaliwa na mataifa mawili.

Kabla ya Brazil kupokezwa uenyeji wa Copa America mwaka huu, kulishuhudiwa pingamizi nyingi zilizowasilishwa mahakamani na washikadau mbalimbali wakiwemo wanasoka Henrique Casemiro wa Real Madrid na Neymar Jr wa Paris Saint-Germain (PSG).

Hata hivyo, majaji wa Mahakama ya Juu nchini Brazil walitupilia mbali maombi yaliyokuwa yamewasilishwa kortini kuzuia fainali za kipute hicho kuandaliwa nchini humo kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa mujibu wa malalamishi, ilihojiwa kwamba maelfu ya raia na wakazi wa Brazil walikuwa katika hatari ya kuambukizwa corona iwapo fainali za Copa America zitaandaliwa nchini humo. Hata hivyo, majaji walishikilia kwamba Katiba ya Brazil haina uwezo wa kushinikiza korti kutoa amri ya kusitishwa kwa maandalizi ya kivumbi hicho.

Badala yake, walitaka magavana na mameya wa miji mikuu kuhakikisha kwamba kanuni zote za kudhibiti maambukizi corona zinazingatiwa katika himaya zao.Vikosi vinavyoshiriki Copa America vitakuwa vikifanyiwa vipimo vya corona kila baada ya saa 48 huku wachezaji na maafisa wa vikosi vyao wakinyimwa uhuru wa kutembea ovyo.

Kivumbi cha Copa America kilichokuwa kifanyike mnamo 2020, kiliahirishwa kwa sababu ya corona ambayo imesababisha zaidi ya vifo 480,000 nchini Brazil.Brazil walishinda Venezuela 1-0 walipokutana mara ya mwisho mnamo Novemba 2020 katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Japo mechi ya leo inawapa Venezuela jukwaa mwafaka la kujinyanyua baada ya kushinda mchuano mmoja pekee kati ya sita iliyopita, watakuwa bila mshambuliaji wao tegemeo, Salomon Rondon anayeuguza jeraha.

Mapema mwezi huu, Venezuela walitia kapuni alama moja pekee kutokana na mechi mbili za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia baada ya kupepetwa 3-1 na Bolivia kisha kuambulia sare tasa dhidi ya Uruguay.

  • Tags

You can share this post!

Aliyetishia kumuua mpenziwe ahukumiwa

Mhudumu wa bodaboda anusurika kifo kwa kichapo