• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Ujerumani watoka nyuma na kupepeta Ureno 4-2 kwenye gozi kali la Euro

Ujerumani watoka nyuma na kupepeta Ureno 4-2 kwenye gozi kali la Euro

Na MASHIRIKA

UJERUMANI walitoka nyuma na kuwapokeza Ureno ambao ni mabingwa watetezi wa Euro kichapo cha 4-2 katika mechi ya Kundi F iliyowakutanisha uwanjani Allianz Arena mnamo Jumamosi.

Matokeo hayo yaliweka wazi Kundi F kwa kikosi chochote kuibuka kileleni.

Ujerumani na Ureno sasa wanajivunia alama tatu kila mmoja huku Ufaransa waliolazimishiwa na Hungary sare ya 1-1 katika mechi nyingine ya Jumamosi, wakidhibiti kilele kwa pointi nne.

Beki Robin Gosens anayechezea Atalanta ya Italia aligeuka tegemeo kubwa la Ujerumani baada ya kuchangia bao na kufunga jingine dhidi ya Ureno.

Mvamizi na nahodha Cristiano Ronaldo aliwafungulia Ureno ukurasa wa magoli katika dakika ya 15 kabla ya beki Ruben Dias wa Manchester City kusawazishia Ujerumani alipojifunga katika dakika ya 35.

Bao la pili la Ujerumani pia lilitokana na Ureno kujifunga kupitia kwa Raphael Guerreiro kunako dakika ya 39. Magoli hayo mawili yalichochea motisha ya Ujerumani waliofunga mabao mawili mengine ya haraka kupitia kwa Kai Havertz na Gosens katika dakika za 51 na 60 mtawalia.

Ingawa Ureno walipania kurejea mchezoni kupitia goli la Diogo Jota katika dakika ya 67, juhudi zao ziliambulia pakavu.

Bao la Ronaldo anayechezea Juventus lilikuwa lake la tatu kufikia sasa kwenye kampeni za Euro mwaka huu na la 12 katika historia yake ya kushiriki kipute hicho cha bara Ulaya.

Ronaldo sasa amepachika wavuni magoli 107 akivalia jezi za timu ya taifa ya Ureno ambao wamemwajibisha mara 177. Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid sasa amesalia na magoli mawili pekee kumfikia Ali Daei wa Iran ambaye mabao yake 109 kimataifa ndiyo rekodi ya dunia.

Ujerumani ambao ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia sasa watakamilisha kampeni zao za Kundi F dhidi ya Hungary mnamo Juni 23 huku Ureno wakivaana na Ufaransa.

Baada ya Ujerumani kupigwa 1-0 na Ufaransa katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi F, kocha Joachim Loew aliwataka wavamizi wake kujituma zaidi na wawe wakiendea mabao ya mapema dhidi ya wapinzani wao.

Katika jitihada za kuzingatia maagizo hayo ya kocha wao, Ujerumani walianza mechi kwa matao ya juu huku bao la Gosens chini ya dakika 10 za mwanzo wa kipindi cha kwanza likikataliwa na refa kwa madai kwamba alicheka na nyavu za Ureno akiwa ameotea.

Ujerumani hawajawahi kupoteza mechi mbili za ufunguzi wa kipute chochote cha haiba kubwa kwa mfululizo tangu mwaka wa 2000 ambapo walikung’utwa na Uingereza na Ureno kwenye fainali za Euro. Walivuta mkia wa kundi lao mwaka huo.

Loew aliteua kudumisha kikosi kilichocheza dhidi ya Ufaransa huku Gosens, Havertz na Joshua Kimmich wakiwatatiza sana madifenda wa Ureno.

Fainali za Euro mwaka huu ni kipute cha mwisho kwa kocha Loew kusimamia katika timu ya taifa ya Ujerumani ambayo amekuwa akiinoa kwa miaka 15 iliyopita. Licha ya Ujerumani kubanduliwa mapema kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, Ujerumani walihiari kusalia na Loew, 61.

Ingawa hivyo, kocha huyo ataondoka sasa mnamo Julai na nafasi yake kutwaliwa na aliyekuwa mkufunzi wa Bayern Munich, Hansi Flick.

Ureno hawajawahi kushinda mechi yoyote ya Euro ambayo imewashuhudia wakiwa chini kwa mabao kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza. Kichapo kutoka kwa Ujerumani kiliwafanya Ureno kuwa mabingwa watetezi wa kwanza wa Euro kuwahi kufungwa mabao manne katika mechi moja.

Ureno watajibwaga ugani dhidi ya Ufaransa katika mechi ijayo wakiwa na ulazima wa kushinda au kusajili sare ili kufuzu kwa hatua ya 16-bora. Mechi hiyo itarejesha kumbukumbu za fainali ya 2016 ambapo Ureno waliwapiku wenyeji Ufaransa jijini Paris.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AKILIMALI: Ana mpango wa kutengeneza soseji za samaki...

Ufaransa wakabwa koo na Hungary katika mchuano wa Euro