• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 3:19 PM
AKILIMALI: Ana mpango wa kutengeneza soseji za samaki kubuni nafasi za kazi

AKILIMALI: Ana mpango wa kutengeneza soseji za samaki kubuni nafasi za kazi

Na SAMMY WAWERU

JE, ulifahamu kuwa soseji zinaweza kutengenezwa kwa nyama zingine mbali na unayojua?

Teknolojia na mambo yanavyoendelea kuboreka ndivyo uvumbuzi mgeni unaibuka.

Patrick Kamau ni mfugaji wa samaki eneo la Kiamumbi, mtaani Kahawa West, kiungani mwa jiji la Nairobi.

Kamau na ambaye ni mwathiriwa wa vita na ghasia za baada ya uchaguzi wa 1992, amejaribu miradi kadha ya ufugaji, ila huu wa samaki umemuitikia na kumkubali.

Aliuingilia mwaka wa 2006, baada ya kufanya utafiti uliomfungua macho.

“Nilitazama programu kwenye runinga, na kugundua ufugaji wa wanyama wa majini ninaofuga hawana gharama. Samaki hula gramu 0.02 ya chakula, ya uzito wake,” Kamau anasema.

Isitoshe, ni vigumu samaki kuugua wala kushambuliwa na vimelea au wadudu. Wanachohitaji ni kudumisha kiwango cha hadhi ya juu cha usafi kidimbwini na katika mazingira.

Patrick Kamau ni mfugaji wa samaki eneo la Kiamumbi, mtaani Kahawa West, Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

“Muhimu zaidi ni maji yawe safi na pia chakula,” anahimiza mfugaji huyu.

Francis Faluma, mtaalamu wa masual ya samaki na afisa katika idara ya ufugaji wa samaki Kaunti ya Kakamega ashauri haja ya kuwalisha chakula kilichosheheni Protini.

“Samaki hukua kwa kasi na wenye afya bora wakilishwa chakula chenye madini ya Protini,” Faluma asema.

Huku mradi wa Kamau maarufu kama Kiamumbi Fish Farm, ukiwa na vidimbwi 49, pia huchoma na kukaanga samaki.

Ana mkahawa wa shughuli hiyo eneo la Kahawa West na Ruiru alamaarufu Tango Gardens, huduma ambazo alianza miaka kadha iliyopita.

“Wateja walianza kunihimiza niwe nawakaangia, si wengi wanaojua kuchoma na kukaanga samaki,” aelezea, akiongeza kuwa shughuli hiyo imebuni nafasi za ajira kwa vijana kadhaa.

Huandamanisha samaki kwa ushumbi wa ugali na mboga za kienyeji anazokuza katika bustani lake.

Mwaka wa 2018, Kamau anaiambia Taifa Leo kwamba aliingiwa na wazo la kuongeza samaki thamani, kupitia utengenezaji wa soseji.

Huku akiendelea kujiandaa kwa mradi huo na ambao huenda ukatikisa taifa, anafichua amenunua mashine za shughuli hiyo.

“Nilichukua mkopo kuwekeza katika mashine za kusindika samaki, kuunda soseji,” adokeza.

Mlipuko wa janga la Covid-19 mwaka uliopita, hata hivyo ulisimamisha mipango hiyo.

“Ninatumai mambo yakiimarika, nitaanza utengenezaji wa soseji za samaki. Kwa sasa mashine zimelala kwenye ghala,” anasema akilalamikia kuathirika pakubwa na virusi vya corona.

Ugonjwa wa Covid-19, ambao sasa ni janga la kimataifa umeyumbisha sekta zote, ile ya huduma za hoteli na utalii ikionekana kulemewa zaidi, hasa kutokana na amri kudhiti idadi ya wateja wanaohudumiwa mara moja na pia kafyu.

“Covid-19 imesambaratisha mikakati niliyokuwa nimeweka. Ninaendelea kulipa mkopo niliochukua kwa minajili ya kununua mashine za kutengeneza soseji za samaki,” asema.

Mjasirimali huyu hata hivyo ana imani mambo yatarejelea yalivyokuwa awali, akiihimiza serikali kujali maslahi ya wafanyabiashara wa kiwango kidogo na kile cha kadri, ndio SMEs.

“Nikianza kutengeneza soseji kwa kutumia nyama za samaki, nafasi za kazi kwa vijana wetu zitajiri. Utakuwa mradi wa kipekee na ambao utatikisa mawimbi ya biashara nchini,” asisitiza.

Uongezaji thamani katika mazao ya kilimo na ufugaji, unatiliwa mkazo ili kuboresha bei ya bidhaa.

“Nyama zinapoongezwa thamani bei huwa bora. Kwa mfano, kero ya kusafirisha mifugo hadi jijini Nairobi ili kuwahi soko, tunapangia kuitatua kwa kuzindua vichinjio mashambani wanakofugwa ng’ombe, mbuzi na kondoo ili kusafirisha nyama na pia kuziongeza thamani,” Katibu katika Wizara ya Mifugo, Harry kimtai akaambia Taifa Leo majuzi kwenye mahojiano ya kipekee afisini mwake, Kilimo House, jijini Nairobi.

Alisema wizara yake tayari inaendelea na mipango ya miradi hiyo katika kaunti kame, na ambazo zinategemewa kwa nyama ya mifugo.

You can share this post!

Argentina walambisha Uruguay sakafu kwenye mechi ya Copa...

Ujerumani watoka nyuma na kupepeta Ureno 4-2 kwenye gozi...