• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kamati yaonya Knec kuhusu jengo lililokwama

Kamati yaonya Knec kuhusu jengo lililokwama

Na SAMWEL OWINO

Jengo moja lililochukua miaka 33 bila kukamilika, limetengewa Sh500 milioni zaidi katika bajeti ya mwaka huu, huku wabunge wakionya kuchukuliwa hatua lisipokamilika.

Jengo hilo ambalo ni Makao Makuu ya Baraza la Mitihani la Kenya(KNEC) lililoanza kujengwa 1986 lilitengewa Sh 395 milioni katika bajeti mbadala ya mwaka 2019/2020.

Kamati ya Elimu ya Bunge iliwalaumu baadhi ya watu wanaojifaidi na pesa za mradi huo kwa kutokamilika kwa jengo hilo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Bi Florence Mutua alisema, kuna watu wachache wanaonufaika kutokana na mradi huo.

“Ni aibu kwa wachache kutaka hali kubaki ilivyo. Jengo hilo lazima likamilishwe ili kuokoa zaidi ya Sh 110 milioni zinazotumika kukodisha vyumba na matumizi mengine, kando na uchapishaji wa mtihani unaofanyika Uingereza ambayo ni gharama zaidi,” alisema Bi Mutua.

Mwakilishi huyo wa Wanawake wa Kaunti ya Busia alisema idadi ya gharama ya kuchapisha mitihani itapanda kutokana na mfumo mpya wa elimu, unaohitaji mitihani mingi.

“Katika bajeti ijayo, kitakachohitajika ni pesa za kununua mashini za kuchapisha mitihani ili kulinda ushuru wa mwananchi,” Bi Mutua aliongeza.

Wabunge walilalamikia kutokamilishwa kwa jengo hilo licha ya kutengewa mamilioni ya pesa katika bajeti ya kila mwaka.

“Miaka 33 ni muda mrefu kwa mradi kama huo. Masuala kama haya yanafaa kuchunguzwa na Kamati ya Bajeti kwa sababu yanatumia pesa za umma visivyo,” akasema Mbunge wa Kisauni, Ali Mbogo.

Kamati ya Bajeti ilionya wizara za serikali na mashirika dhidi ya kuanza miradi mipya kabla ya kukamilisha inayoendelea.

You can share this post!

Kashfa ya vyama kadha kusajili raia kwa lazima yakera...

Ruto akejeli muungano wa Uhuru na Raila