• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KAMAU: Himaya za kifalme hazina nafasi sasa

KAMAU: Himaya za kifalme hazina nafasi sasa

Na WANDERI KAMAU

MFUMO wa utawala wa kifalme ulikuwa njia iliyojenga uthabiti wa kisiasa katika mataifa mengi karne nyingi zilizopita.

Ufalme ulionekana kuwa msingi uliojenga umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa jamii nyingi ambazo ziliegemea mfumo huo.

Chini ya mfumo huo, jamii ziliendesha masuala mengi kwa umoja, hali iliyoziwezesha kupata ufanisi mkubwa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.

Ni kupitia umoja huo ambapo falme husika zilipata nguvu za kisiasa, hasa kwenye matukio kama vita.

Falme zilizopata ufanisi zilikita hatua hizo na aina ya wafalme zilizokuwa nao.

Ingawa mfumo huo ulikuwa maarufu sana katika baadhi ya nchi za Ulaya Magharibi na Asia Mashariki, mtindo huo ulianza kubadilika kadri nyakati zilivyosonga.

Mataifa mengi kama Ufaransa yaliacha kuzingatia mfumo huo, baada ya maasi makubwa yaliyotokea kuupinga mwishoni mwa karne ya 18.

Hata hivyo, baadhi ya nchi kama Norway, Ubelgiji na Uingereza zimeendelea kuuzingatia—lengo kuu likiwa kuendeleza umoja miongoni mwa jamii na makundi mbalimbali.

Barani Afrika, mfumo huo ulibadilika kabisa kadri nchi nyingi zilivyoendelea kupata uhuru kutoka kwa wakoloni miaka ya sitini.

Kabla ya ujio wa Wakoloni, karibu jamii zote barani humu zilikita mitindo yake ya uongozi katika mfumo wa kifalme.

Moja ya sababu ambapo jamii nyingi huzingatia demokrasia ni kuwa, kinyume na ufalme, demokrasia huwa inatoa nafasi kwa wanajamii kuwachagua viongozi wanaowataka.

Kando na hayo, jamii huwa na nafasi ya kuwauliza viongozi hao maswali kuhusu masuala inayodhani hawajayawajibikia ifaavyo.

Licha ya mfumo wa ufalme kuonekana kama ishara ya kuendeleza umoja, baadhi ya wafalme wamekuwa wakiutumia kama njia ya kujitajirisha ama kuelekeza raslimali za nchi husika kwa maslahi yao wenyewe, bila kujali hali ya wanajamii wengine.

Taswira hiyo ndiyo inayoshuhudiwa kwa sasa nchini eSwatini (Swaziland), ambayo ni miongoni mwa mataifa machache barani Afrika yanayozingatia mfumo wa kifalme.

Kwa muda mrefu, Mfalme Mswati III amekuwa akilaumiwa kwa kutumia raslimali za taifa hilo dogo kujitajirisha na kujifurahisha atakavyo.

Kila mwaka, imekuwa kawaida kwa mfalme huyo “kumchagua” mke mpya miongoni mwa mamia ya wasichana ambao hujitokeza kucheza densi mbele yake wakiwa kifua wazi.

Ingawa ni hafla ambayo hufasiriwa kama “mwendelezo wa tamaduni” za wenyeji, huu ni mtindo ambao kamwe haulingani na mwelekeo wa kimaisha katika karne ya 21.

Ni sababu hiyo ambapo maasi dhidi ya utawala huo yamekuwa yakiongezeka kutoka kwa wanaharakati wa demokrasia.

Licha ya utawala huo kufanya kila uwezalo kuwanyamazisha wanaharakati hao, juhudi hizo zinaonekana kukaribia kuzaa matunda.

Demokrasia inaendelea kukumbatiwa na jamii nyingi kote ulimwenguni.

Baadhi ya wadadisi wanasema kuwa hata nchini Uingereza, huenda hali ikaanza kubadilika baada ya kipindi cha Malkia Elizabeth kukamilika.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Vyama vya kisiasa viwe na ukomavu

KINYUA BIN KING’ORI: Wapigakura wa kulaumiwa kuchagua...