• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
SHINA LA UHAI: HIV: Maelfu wakwepa tembe za PrEP, kunaendaje?

SHINA LA UHAI: HIV: Maelfu wakwepa tembe za PrEP, kunaendaje?

Na LEONARD ONYANGO

USIPOKUWA makini utadhani tembe ya kuzuia virusi vya HIV, pre-exposure prophylaxis (PrEP), ni sawa na tembe ya kupunguza makali ya virusi hivyo mwilini, antiretroviral (ARVs). Hii ni kwa sababu tembe hizo mbili zinakaribiana kufanana kwa rangi na ukubwa.

Tembe za PrEP humezwa kila siku na watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa HIV ili kupunguza uwezekano wa maambukizi.

Makundi ya watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa HIV ni watu walio na wapenzi zaidi ya mmoja, wanandoa ambao mmoja wao anaishi na virusi, wanaofanya kazi ya ukahaba, mashoga kati ya wengineo.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu akimeza PrEP kila siku anapunguza uwezekano wa kuambukizwa HIV kwa asilimia 90.

Bodi ya kudhibiti Dawa na Sumu nchini (KPPB) iliidhinisha matumizi ya PrEP kuzuia maambukizi ya HIV humu nchini mnamo 2015.

Shirika la WHO linasema kuwa ARVs zikimezwa kila siku kwa kuzingatia maagizo ya daktari, virusi vinaweza kupungua kwa kiasi kikubwa mwilini na mwathiriwa aishi maisha ya kawaida sawa na watu wengine.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Wakenya milioni 1.6 milioni wanaoishi na virusi vya HIV, wanatumia tembe za ARVs.

Watu 42,000 huambukizwa virusi vya HIV nchini Kenya kila mwaka.

Lakini kufanana kwa tembe hizo mbili kumesababisha baadhi ya watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya HIV kukwepa kutumia PrEP.

Carol ambaye anafanya kazi ya ukahaba jijini Nairobi anasema alijipata pabaya mteja wake alipopata tembe za PrEP ndani ya mkoba wake.

“Alidhani tembe hizo zilikuwa ARVs. Alinizaba kofi na kisha kuondoka na simu yangu,” anasema.

Anakiri kuwa kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kuweka kafyu ya usiku ambayo imekuwepo kuanzia Aprili mwaka jana, alikuwa akijipatia wateja wasiopungua wanne kwa usiku mmoja hususani siku ya Ijumaa.

Kati ya wanne hao kuna uwezekano mkubwa kwamba mmoja wao ana virusi vya HIV.

Aidha anasema tangu aliposhambuliwa na mteja wake, alibadili mbinu – hatembei na tembe hizo tena kwenye mkoba wake.

“Ninameza kila siku asubuhi kwa kutumia chai au uji na kisha ninaziacha nyumbani. Sitembei nazo tena,” anasema.

Lakini anafichua kuwa wengi wa marafiki zake wameacha kuzitumia baada ya kushambuliwa au kunyanyapaliwa na wateja wao.

“Wengi wao wanatumia mipira ya kondomu kujikinga. Lakini tatizo la kondomu ni kwamba ukiwa mlevi na ushiriki mapenzi itakuwa vigumu kumshinikiza mteja kutumia kinga. Kwa hivyo, tembe ya PrEP inafaa zaidi,” akasema.

Baadhi yao anasema, wanameza tembe za post-exposure prophylaxis, maarufu PEP baada ya kushiriki mapenzi.

Tembe za PEP humezwa baada ya kushiriki na mtu unayemshuku kuwa na virusi vya HIV.

Wataalamu wanashauri kuwa PEP zinafaa kuanza kumezwa ndani ya saa 72 baada ya kushiriki ngono na baadaye uendelee kumeza kwa siku 28.

Aidha wanashauri tembe ya PrEP na kondomu zitumiwe kwa pamoja ili kuzuia maambukizi ya HIV na maradhi mengineyo ya zinaa kwa asilimia 100.

Steve ambaye ni mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, anasema kuwa hana ufahamu kuwa tembe za PrEP zinafaa kutumiwa na wanaume pia.

“Ninachojua ni kwamba PrEP zinatumiwa tu na wanawake, haswa wanaofanya biashara ya ukahaba. Sijawahi kuona mwanaume akizimeza,” anasema Steve huku akicheka.

Anasema kuwa mara kwa mara amekuwa akitumia kondomu kujikinga virusi vya HIV.

Lakini anakiri kuwa mara nyingine hushindwa kutumia kondomu hivyo kujitia katika hatari ya kuambukizwa virusi vya HIV.

Tembe za PrEP hutolewa bila malipo katika hospitali za umma katika kaunti zote 47.

Ripoti

Ripoti ya Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Kudhibiti Ukimwi na Maradhi ya Zinaa (NASCOP) ya 2018 inaonyesha kuwa Kaunti ya Homa Bay inaongoza kwa kuwa na vituo vingi vya kutoa tembe za PrEP.

Kulingana na ripoti hiyo, vituo vinavyotoa PrEP katika Kaunti ya Homa Bay ni 156, Siaya (140), Nyamira (140), Kakamega (56) na Kisumu (73).

Kaunti ya Nairobi inayoongoza kwa idadi ya watu, ina vituo 73 vya kutoa tembe hizo za kuzuia maambukizi ya HIV.

Kaunti za Tharaka Nithi, Nyandarua, Samburu, Pokot Magharibi, Isiolo, Lamu, Taita Taveta na Marsabit zina chini ya vituo 10 vya kutoa PrEP kila moja.

Karibu nusu (asilimia 47) ya wanaotumia tembe za PrEP ni wanandoa ambao mmoja wao anaishi na virusi vya HIV, vijana (asilimia 12), makahaba wa kike (asilimia 12) na watumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga sindano (asilimia 0.2) kati ya wengineo.

Ripoti hiyo ilibaini kuwa wengi wa wanaotumia PrEP humu nchini wako chini ya umri wa miaka 40.

Asilimia 65 ya wanaotumia tembe za PrEP ni wanawake na wengi wao ni wa umri wa kati ya miaka 20-24.

Ripoti ya NASCOP inaonyesha kuwa karibu asilimia 50 ya waliokuwa wakitumia PrEP kabla ya Oktoba 2018, wameacha.

Kati ya watu 46,000 waliokuwa wakitumia PrEP kabla ya Oktoba 2018, ni 23,000 ambao wanaendelea kutumia tembe hizo humu nchini kufikia sasa.

Kaunti za Kisumu na Nairobi zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ambao wanatumia PrEP kwa muda mfupi na kuacha.

WHO lililenga kuhakikisha kuwa idadi ya watu wanaotumia PrEP kote ulimwenguni wanafikia milioni 3 kufikia mwishoni mwa 2020. Lakini idadi hiyo ingali chini ya milioni 1.

Profesa Nelly Mugo, mtafiti wa masuala ya HIV katika Taasisi ya Kutafiti Dawa nchini (Kemri) anasema kuwa unyanyapaa unasukuma wengi kuacha kutumia tembe ya PrEP.

“Utafiti tuliofanya ulibaini kwamba watu wengi wanaona haya kutumia PrEP mbele ya wapenzi wao kutokana na hofu kwamba huenda wakadhaniwa kuwa wana virusi vya HIV. Hii ni kutokana na ukweli kwamba tembe za PrEP zinafanana na zile za ARVs,” anasema.

Prof Mugo anasema baadhi ya watu wanaacha pia kutumia tembe hizo kwani ni vigumu kuzimeza kila siku.

Prof Mugo ambaye hivi karibuni alitunukiwa tuzo ya Gita Ramjee kwa kuwa mtafiti wa kike aliyefana katika utafiti wa kuzuia maambukizi ya HIV, ni miongoni mwa watafiti wanaofanya awamu ya tatu ya majaribio tembe ya Islatravir ambayo inamezwa mara moja kwa mwezi.

Islatravir humezwa mara moja kila baada ya siku 30 na wataalamu wa afya wanaamini kuwa huenda ikakumbatiwa zaidi na mamilioni ya watu ikilinganishwa na PrEP.

Majaribio hayo yatahusisha wanawake 4,000 katika mataifa ya Kenya, Afrika Kusini, Uganda, Malawi, Eswatini, Zimbabwe na Zambia.

Majaribio ya mwanzo yalionyesha kuwa tembe moja ina uwezo wa kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV kwa kipindi cha mwezi mmoja.

You can share this post!

Lengo la Uingereza kwa sasa ni kutwaa Kombe la Dunia 2022...

Makomando wawinda Kangogo