• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:10 PM
MWANAMUME KAMILI: Ndoa thabiti ni msingi wa familia na jamii endelezi

MWANAMUME KAMILI: Ndoa thabiti ni msingi wa familia na jamii endelezi

Na DKT CHARLES OBENE

LEO tunatia guu katika uchanganuzi wa suala tata la ndoa.

Wangwana wamekwisha kutudokezea kwamba ndoa thabiti ndio msingi wa jamii endelezi. Je, maoni yako yanawiana ama yanakinzana na kauli hiyo?

Japo tupo shinani mwa teknolojia na teknohama lakini tusije asi maadili na kanuni zinazoelekeza sawia na kuongoza ndoa.

Hatuna budi kusimama wima kuhimiza nidhamu na adhabu kwenye jamii. Ama sivyo wanavyofanya wangwana walioangaziwa na nyota jaha?

Itakuwa hatari mno kwa jamii zijazo ikiwa suala la ndoa litaachiwa kuamuliwa na majanadume wa leo waliojawa ashiki na tamaa ya maumbo yanayozinga.

Wakiona dodoki wanaanza ndondokwa hawajamjua mwanamtu atokako wala aendako. Hapo kuna hatari na shari maradufu. Itakuwa hatari zaidi kuwaachia majanajike pekee kuamua jinsi watakavyoolewa.

Wakishaona mizinga mahambe hawa watagutuka punde wamekwisha himilika hawajui vipi na wapi ndimi za ashiki kuwashikisha mafua wakaugua japo hawana hanani.

Jinsi wanavyobeba simu na vipakatalishi, wanadhani hata ndoa ni miongoni mwa vifaabebe kuchupia kisha kuchepuka kama wanadamu wendao kilingeni.

Hawana hekima hawana stahamala mambo kuyasuka, yakaiva taratibu.

Kama pomboo majini, wanafyatuka hawajakolea hawajakoleza tui. Wanastahili mwongozo na mwelekeo watu hawa. Wanastahili hekima ya wazazi wanaojua maana na hadhi ya ndoa. Ndoa thabiti ni msingi wa jamii endelezi.

Je, ipi sawa kati ya ndoa zenye msingi wa kidini na zile zinazoasisiwa kizani zenye mfumo wa “njoo tuanze maisha?” Mjadala umekuwepo, upo na bado utakuwepo juu ya suala la ndoa.

Haidhuru! Lazima tuyaweke wazi mambo yanayostahili kudhihiri maishani mwa mume na mke mwema. Mambo ya ndoa ni wajibu wa familia na jamii nzima. Mzazi yupi angependa bintiye kuchumbiwa na mlofa asiyejua be wala te? Yaani mwanao aondoke tu jioni kwenda ziarani halafu asirudi tena nyumbani kwa kuwa “ameolewa!”

Wangapi wangependa kupokea tu arafa kutoka kwa binti kwamba “msinitafute maana nimekwisha olewa?”

Hebu tafakari fikira zinazokita akilini mwa baba na mama ambao hukumbana na dhoruba ya “binti kuhimilika angali sebuleni kwa wazaziwe!”

Nawapongeza mno wazazi wanaofanya kila jitihada kuhakiki mustakabali wa watoto angalau kuwapa msingi wa ndoa thabiti. Yote haya yanafanyika ili kuheshimu mila na tamaduni, kuzuia fedheha na kudumisha hadhi ya familia na jamii.

Jitihada hizo zinaashiria umuhimu wa ndoa thabiti katika kuendeleza maadili kwenye jamii. Nakumbuka vyema kauli ya mzazi mmoja alipomweleza bintiye “kama niliolewa gizani nikawazaa vilabuni hamna budi kunitenda vivyo hivyo!” Hakutumia kiboko wala ugomvi na wanawe, lakini sauti ile ya mama imewakita akilini hadi leo!” Je, wangapi wana muda kutoa mwelekeo kwenye jamii jinsi alivyofanya mwanamke yule?

Usuhuba na uchumba unaweza kuendeshwa kisirisiri, wangwana kukutana kizani hata wakasalitika na kuwehuka kwenye tanuri la mahaba bila mtu kujua. Mwanzo wa ngoma ni lele. Wajua tena athari ya urembo unaosisimua hadi mja anapagawa! Ama sivyo wanavyojitetea wanaume? Wanajua sana kujitetea hasa wanapoishiwa subira wakajongea mekoni, wakapakua japo chakula hakijaiva na mwanamtu kuishia pajani kupakatwa kabla ya posa. Ndio mtindo wa leo eti.

Tuacheni michezo ya siri tukite kwenye uhalisia. Ijapo timia wakati wa janadume kuoa ama janajike kuolewa sharti khanga za siri kuvuliwa, mambo yakawekwa wazi tena peupe. Raha ya ndoa kama ngoma za kitamaduni, ni mrindimo! Hakuna siri wala cha siri kwenye ndoa. Hili litue na kukolea akilini mwa wachumba wanaotaka ama wanaodhamiria kuasisi familia. Ninasema “kutaka” na “kudhamiria” nikijua tosha kwamba sio wote wanaotaka wana dhamira. Isitoshe, ndoa ndio asili fasili ya familia nayo familia thabiti ndio kiini na msingi wa jamii thabiti. Hatuna budi kuwa watu wema wanaotaka tena wanaodhamiria mema. Dhamira ni sehemu ya ndoa.

Ndoa za kidini ama “njoo tuanze maisha?” Hili ni swali linalostahili kuangaziwa, kuzungumziwa na kujadiliwa kimasomaso kwa kuwa suala la ndoa linaathiri sio tu wanandoa bali pia familia na jamii husika. Uamuzi wa janadume kuoa ama janajike kuolewa sio wazo la janajike ama kauli ya janadume tu. Huu ni mzigo ambao daima hutulia begani mwa familia na jamii kwa jumla. Tukubaliane kwamba ndoa zinazoasisiwa juu ya msingi wa maadili daima hudumu tena hunawiri mfano wa mche ulioatikwa kwenye rutuba. Mavuno yatokanayo kwenye ndoa hizo adilifu ni mengi kwa familia na jamii. Kwa msingi huo huo, ndoa zisizozingatia kanuni na maadili mema ya jamii hukumbwa na changamoto si haba.

Kuchagua mume ama mke ni jambo la mtu binafsi. Uamuzi na kanuni za ndoa ni suala linalohusu familia na jamii. Mume ama mke ni jambo la mtu binafsi. Tusijekuwa wezi kuolewa gizani halafu tukimbilie kwa wazazi kutafuta patanisho nyakati za dhiki.

[email protected]

You can share this post!

Waziri apongeza Lionesses kujikatia tiketi ya fainali ya...

UMBEA: Si kila wivu ni mbaya, wakati mwingine hujenga...