• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Machifu walivyopora mabilioni ya Covid

Machifu walivyopora mabilioni ya Covid

Na NDUNGI MAINGI

KIASI kikubwa cha Sh10 bilioni zilizotolewa na serikali kusaidia familia maskini kupambana na makali ya janga la corona kiliishia katika mifuko ya maafisa walioendesha shughuli hiyo hasa machifu na jamaa zao, inasema ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa jana jijini Nairobi, inasema msaada huo wa kifedha ulifikia asilimia 4.8 pekee ya watu waliopitia hali ngumu ya maisha wakati wa janga hilo, baada ya wengi kupoteza ajira na biashara kuporomoka.

“Inasikitisha kuwa mpango mzuri kama huo unaweza kuharibiwa kutokana na mwenendo wa kutojali na usimamizi mbaya. Serikali inafaa kuwahahakikishia wananchi kuwa uchunguzi utaanzishwa kuhusu suala hili,” alisema mkurugenzi wa shirika hilo, tawi la Afrika Mashariki, Atsieno Namwaya.

Waziri wa Fedha na Mipango, Bw Ukur Yatani, alieleza shirika hilo kuwa serikali ililenga zaidi maeneo yenye umaskini mkubwa, na hasa familia ambazo zilikabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile magonjwa hatari na ulemavu.

Hata hivyo, uchunguzi wa shirika hilo uligundua kuwa baadhi ya machifu na maafisa wa ngazi za juu walikiuka maagizo ya serikali kwa kuwasajili marafiki na jamaa zao, baadhi wakiwa watu wanaojiweza kiuchumi na waajiriwa wa ofisi zao.

Baadhi ya machifu walifichua kuwa walishinikizwa na maafisa wa ngazi za juu serikalini kusajili idadi ndogo ya waliolengwa ili marafiki zao waweze kunufaika.Baadhi ya wakazi katika mitaa ya Kibra na Mathare jijini Nairobi pia walifichua kuwa idadi ya waliofaidika haiwiani na idadi iliyotangazwa na serikali.

Pia baadhi walipata pesa hizo kwa awamu mbili au tatu pekee, kinyume na ripoti ya serikali kwa iliwapa pesa hizo kila wiki hadi Novemba mwaka jana.“Ripoti ya serikali ilieleza kuwa pesa hizo zilitolewa tangu Aprili 22 hadi Novemba 27.

Hata hivyo, baadhi walipokea pesa hizo kufikia miezi ya Juni na Agosti. Haijulikani aliyepokea pesa zao wakati uliosalia,” alieleza Bw Namwaya.

  • Tags

You can share this post!

Wahamiaji wazidi kufurika Uingereza

Watu 8 wauawa katika mashambulizi baada ya ziara ya...