Wakenya Hamza Anwar, McRae Kimathi na Jeremy Wahome wawania taji la mbio za magari Tanzania

Na GEOFFREY ANENE

MADEREVA Hamza Anwar, McRae Kimathi na Jeremy Wahome, ambao wako katika mradi wa chipukizi kukuzwa na Shirikisho la Mbio za Magari Duniani (FIA), wamejaa matumaini ya kufanya vizuri kwenye duru ya tatu ya Afrika nchini Tanzania mnamo Julai 23-25.

Wakenya hao wanaodhaminiwa na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom na ile ya ndege ya Kenya Airways, walielekea Tanzania mapema Julai 21 kwa duru hiyo ambayo imevutia makumi ya madereva kutoka mataifa ya Kenya, Tanzania, Uganda na Afrika Kusini.

Wahome,22, Anwar,22, na Kimathi,26, walishiriki duru ya sita ya Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally nchini Kenya mnamo Juni 24-27. Akielekezwa na Victor Okundi, Wahome alimaliza katika nafasi nzuri ya 16.

Anwar na mwelekezi wake Riyaz Ismail walikamilisha Safari Rally katika nafasi ya 25 naye Kimathi akishirikiana na Mwangi Kioni alijizulu katika mkondo wa 18, hatua chache kabla ya sehemu ya kumalizia mashindano. Wote waliendesha magari ya Ford Fiesta watakayotumia tena nchini Tanzania.

“Nafurahia sana kupata fursa hii kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kushiriki mashindano ya Afrika. Ni mtihani mpya, lakini naamini ujuzi niliopata kutoka kwa Safari Rally utanisaidia kupata matokeo mazuri,” alisema Wahome.

Hamza na Kimathi walishiriki duru ya Afrika ya Equator Rally nchini Kenya mwezi Aprili. Hamza alimaliza katika nafasi ya tano akiendesha gari la Mitsubishi Evo X naye Kimathi akakamata nafasi ya nane. Mshindi wa Equator Rally, Car “Flash” Tundo (Volkswagen Polo) pamoja na Aakif Virani (Skoda Fabia) ni Wakenya mwingine walio Tanzania.