• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
WANDERI KAMAU: Rais Samia amevunja ahadi yake kurejesha demokrasia

WANDERI KAMAU: Rais Samia amevunja ahadi yake kurejesha demokrasia

Na WANDERI KAMAU

TANGU enzi ya hayati Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo zimejizolea sifa ya kuwa tulivu na zenye uthabiti mkubwa kisiasa.

Kinyume na Kenya, Uganda, Ethiopia na nchi nyingine za eneo la Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, Tanzania haijawahi kukumbwa na mapinduzi ya kijeshi.Kenya ilijipata hapo mnamo Agosti 2, 1982, wakati wanajeshi waasi walijaribu kupindua uongozi wa marehemu Daniel Moi.

Uganda imeshuhudia majaribio kadhaa, ambapo viongozi wake wamegeuka kuwa madikteta. Mfano bora ni Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa akitumia nguvu na ushawishi wake kuendelea kukwamilia mamlakani.

Simulizi ni kama hizo katika nchi zilizobaki.Hata hivyo, inasikitisha kuwa Tanzania inarejea katika mwelekeo iliyokuwa chini ya marehemu John Magufuli.

Kati ya mwaka 2015 na 2020, Tanzania iligonga vichwa vya habari kutokana na sera kali alizoanzisha Dkt Magufuli, akiapa “kulainisha na kunyoosya mwelekeo wa taifa hilo kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na uhusiano baina yake na nchi nyingine duniani.

”Licha ya sifa kubwa alizojizolea, Dkt Magufuli aligeuka kuwa kiongozi wa kidikteta.Aliunyamazisha upinzani, kuwahangaisha wanaharakati wa kisiasa na vyombo vya habari.Ni hali iliyotia doa sifa kubwa aliyokuwa amejizolea kama mwanamapinduzi wa kisiasa na mwendelezaji wa tamaduni za Kiafrika.

Magufuli aligeuka kuwa “Musa wa Waafrika” hadi “Msaliti Mkuu wa Demokrasia.”Kwenye hotuba ya kuapishwa kwake mnamo Machi 19, Rais Samia Suluhu Hassan aliapa “kuondoa makosa ya mtangulizi wake.

”Hata hivyo, inaonekana kuwa Rais Suluhu amesahau ahadi alizotoa na badala yake kufuata nyayo za mtangulizi wake.Mnamo Jumatano, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo, CHADEMA, Bw Freeman Mbowe alikamatwa na polisi katika hali tatanishi.

Baada ya kukamatwa, alipelekwa mahali kusikojulikana kwa kisingizio cha kuvunja kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.Licha ya malalamishi kutoka kwa wafuasi wake, serikali imebaki kimya kuhusu aliko kiongozi huyo.

Ingawa ni kawaida kwa serikali kuchukua hatua kuhakikisha sheria na kanuni zilizowekwa zinafuatwa, mwelekeo ambao Tanzania imechukua umeanza kudhihirisha Rais Samia anairejesha katika enzi ya kiimla.

Demokrasia kamili humaanisha kumpa nafasi kila mmoja kujieleza. Si kumtisha anapotafuta nafasi ya kueleza hisia zake.Rais Samia anapaswa kurejelea ahadi yake ya kuondoa makosa aliyofanya Magufuli, ili kuendeleza sifa ya Tanzania kama chemichemi ya demokrasia.

  • Tags

You can share this post!

Sheria Mpya: Madume yalitapeli wanawake!

Kinara wa upinzani Tanzania akabiliwa na kesi ya ugaidi