• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Tufundishwe jinsi ya kuvua samaki na si kuletewa samaki, asema Peter Kenneth

Tufundishwe jinsi ya kuvua samaki na si kuletewa samaki, asema Peter Kenneth

Na SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA mbunge wa Gatanga Peter Kenneth amesuta wanasiasa aliodai wanatoa ahadi zisizoweza kutekelezwa kwa wananchi kwamba pesa ziko za wao kuletewa.

Kenneth kwa upande wake amesema ahadi kama hizo ni hadaa tupu kwa sababu “sisi tuna bidii na tunataka kufundishwa jinsi ya kuvua samaki na wala sio kuletewa samaki.”

“Pesa za serikali huwa hazisambazwi jinsi ambavyo ninaskia wengine wakisema, ati watakuwa wakiwapa wafanyabiashara ili wajiimarishe,” akasema.

Ameonekana kumshambulia Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Jumapili, akizungumza eneo la Nyandarua, Ruto alisema endapo atamrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022, serikali yake itakuwa ikitengea wafanyabiashara mgao wa fedha sawa na Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF).

“Ninapowaeleza ninataka kila mwananchi awe na pesa mfukoni, ninajua ninachosema,” Dkt Ruto akasema.

Kulingana na Bw Kenneth, mgao wa fedha kwa wafanyabaishara unaweza kutekelezwa kupitia serikali za kaunti, kupata nyongeza.

“Nimekuwa katika hazina ya kitaifa, ninaelewa ugavi wa pesa unavyotekelezwa. Fedha za serikali haziwekwi kwenye ghala unaloenda kuzitoa na kuzisambaza unavyotaka,” akasema mwanasiasa huyo ambaye 2017 aliwania ugavana Nairobi, akionekana kuelekeza matamshi yake kwa Naibu Rais.

Bw Kenneth alisema hayo Jumanne kwenye hafla ya wanamuziki iliyoandaliwa eneo la Ndakaini, Kaunti ya Murang’a lakini ambayo kwa asilimia kubwa imesheheni mbwembwe za wanasiasa.

Katika hafla hiyo iliyowaleta pamoja waimbaji kutoka sehemu mbalimbali za nchi na ambapo walitumia jukwaa hilo kuelezea matatizo yao katika ulingo wa muziki, mbunge wa Igembe Kaskazini, Maoka Maore pia alitilia mkazo kauli ya Bw Kenneth.

“Watu milioni 22, itawezekanaje kuwapa Sh100,000 kila mmoja?” Bw Maore akataka kujua.

You can share this post!

Helena Alcinda Panguana ampangua Mkenya Elizabeth Akinyi...

Vipusa wa Amerika watinga robo-fainali za soka ya Olimpiki...