• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
ONYANGO: Nauli zipunguzwe kufuatia agizo la kujaza abiria garini

ONYANGO: Nauli zipunguzwe kufuatia agizo la kujaza abiria garini

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya serikali kuruhusu magari ya usafiri wa umma kujaza abiria kulingana na idadi ya viti kuanzia leo, ni habari njema.

Marufuku ambayo imekuwepo tangu Aprili 2020, ambapo matatu zilitakiwa kubeba abiria asilimia 60 ya uwezo wa gari kwa lengo la kupunguza maambukizi ya virusi vya corona, imewasababishia wananchi mahangaiko tele.

Wahudumu wa matatu waliongeza nauli kwa zaidi ya asilimia 50 ili kufidia viti vilivyokuwa wazi kuepuka hasara.

Kwa mfano, nauli ya kutoka Nairobi hadi mjini Homa Bay iliongezeka kutoka Sh1,000 hadi Sh1,800.

Nauli ya kati ya Kilifi na Nairobi iliongezeka kutoka Sh1,000 hadi Sh1,600.

Kwa sababu matatu zilibeba abiria wachache, wafanyabiashara katika sekta ya usafiri wa umma, vilevile, walilazimika kuongeza idadi ya magari ili kukidhi mahitaji.

Kuongezwa huko kwa magari kulisababisha kuwepo kwa misongamano ya magari katika barabara katika majiji na miji mikuu.

Kuongezwa kwa magari ni hatari kwani yanachafua hewa. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa watu 5,000 hufariki kila mwaka nchini Kenya kutokana na kupumua hewa chafu. Moshi wa magari, haswa makuukuu, unachangia kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa hewa kwa kutoa chembechembe ambazo ni hatari kwa afya.

Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Chris Obure, Ijumaa, aliagiza matatu kuanza kujaza abiria huku akisema kuwa serikali imeafikiana na washikadau katika sekta ya matatu kuhakikisha kwamba masharti ya kujikinga na virusi vya corona yanazingatiwa.

Kulingana na Bw Obure, kila mtu anayeabiri matatu atakuwa ananyunyiziwa ‘sanitaiza’ kuua virusi vya corona.

Ukweli ni kwamba matatu nyingi jijini Nairobi na maeneo mengi ya nchi zimeacha kutumia sanitaiza. Baadhi ya matatu zinatumia sanitaiza feki – ambazo zikinyunyiziwa mikononi inanata kama gundi – ili kubana matumizi.

Bw Obure pia alisema kwamba abiria wote watatakiwa kuvalia barakoa wakati wote. Kuhubiri, kuuza bidhaa na kuombaomba ni marufuku ndani ya magari ya usafiri wa umma.

Sasa macho ya Wakenya yameelekezwa kwa wamiliki wa matatu ikiwa watapunguza nauli au la baada ya kuruhusiwa kujaza magari.

Wahudumu wa matatu wamekuwa na mazoea ya kupandisha nauli bei ya mafuta inapoongezwa. Lakini bei ya mafuta inapopungua nauli inasalia juu.

Serikali inafaa kuweka mipango ya kuadhibu magari ya umma yatakayoendelea ‘kufinya’ abiria kwa kuwatoza nauli ya juu licha ya kuruhusiwa kujaza.

Serikali, vilevile, inafaa kuruhusu safari za usiku kwa mabasi ya masafa marefu ili kuwapunguzia Wakenya mahangaiko. Kafyu inafaa kulegezwa kwa magari ya masafa marefu kwani uwezekano wa abiria kuambukizana virusi vya corona ndani ya basi usiku ni mfinyu mno.

Marufuku ya sasa inamaanisha kuwa ikiwa mtu anasafiri kutoka Kisumu kuelekea Mombasa atalazimika kulala Nairobi hivyo kumuongezea gharama zaidi.

You can share this post!

TAHARIRI: Kila msafiri analo jukumu la kujilinda

WARUI: Mfumo wa CBC ni mzigo kutokana na ughali wa vifaa