• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wafanyabiashara walia ushuru ghali wamnyonga raia

Wafanyabiashara walia ushuru ghali wamnyonga raia

BENSON MATHEKA na WINNIE ONYANDO

WATENGENEZAJI bidhaa nchini wamelaumu wanasiasa kwa kutochukua hatua za kupunguzia Wakenya mzigo wa kupanda kwa gharama ya maisha kunakosababishwa na janga la corona.

Wanasema kwamba asilimia kubwa ya Wakenya wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na athari za janga hilo.

Wakizungumza Jumanne katika mkutano ambao mada yake ilikuwa “Punguza Gharama ya Maisha” wafanyabiashara hao walilalamika kuwa serikali haitoi suluhu kuhusu ufufuzi wa biashara.

Mwenyekiti wa chama cha watengenezaji bidhaa Kenya (KAM), Bw Mucai Kunyiha, alilaumu serikali kwa kuongeza ushuru kiholela bila kujali athari yake kwa umma.

Bw Mucai alisema kupandishwa kwa ushuru kumesababisha mfumko wa gharama ya maisha kwa Wakenya ambao tayari wanalemewa na athari za janga la corona.

“Inakuwa vigumu kufanya biashara nchini Kenya kufuatia kuanzishwa kwa ushuru na ada nyingi,” alisema Bw Mucai katika mkutano uliofanyika jijini Nairobi.

Alitoa mfano wa kanuni za mimea za 2020 zilizoandamana na ada mpya kama hatua ya kudhibiti mimea hiyo.

“Kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2021, serikali ilianzisha ushuru kwa mali-ghafi na ushuru wa ziada wa thamani wa asilimia 16 kwa kusambaza baadhi ya bidhaa na kwa kufanya hivi, ikaongeza gharama ya kufanya biashara na bei kwa wateja,” alieleza Bw Mucai.

“Zaidi ya hayo, serikali imependekeza marekebisho ya asilimia 4.9 ya aina viwango mbalimbali vya ushuru, hatua ambayo itaathiri wateja, watengenezaji bidhaa na kurudisha nyuma hatua zilizopigwa za kuangamiza biashara haramu,” alisema.

Bw Mucai alisema serikali inafaa kufahamu kuwa kuanzishwa kwa hatua hizi kutaathiri sekta tofauti za uchumi.

“Hatua hizi zitaathiri bidhaa zinazotengenezewa nchini na kupunguza mapato ya nchi,” akaongeza Bw Mucai.

Afisa mkuu mtendaji wa Taasisi ya Masuala ya Uchumi (IEA), Bw Kwame Owino, alisisitiza umuhimu wa kuwa na sekta ya kibinafsi inayonawiri.

“Sekta ya kibinafsi ikikosa kukua, ustawi wa uchumi unakwama kwa sababu ya aina nyingi za ushuru wanazostahili kulipa,” akasema Bw Owino.

Kulingana na Bw Owino, Kenya na Afrika kwa jumla inahitaji kulenga ustawi wa uchumi wa kudumu.

“Kama nchi, ni muhimu tukome kupima utendakazi wa ushuru kwa kutegemea viwango vya ushuru tunaokusanya,” akasema Bw Owino.

Naye Afisa Mkuu Mtendaji wa Muungano wa Biashara Ndogo (MSME), Bw Samuel Karanja, alihimiza serikali kuondoa kanuni zilizopitwa na wakati.

Bw Karanja alisema kanuni hizo zinazuia biashara ndogo kustawi.

“Kwa wakati huu, kuna biashara ndogo 7.4 milioni nchini Kenya lakini ni 1.6 zilizo na leseni za kuhudumu. Tunahitaji kurasimisha viwanda vidogo nchini. Kufanya hivi kutahitaji kubuniwa kwa mazingira bora ya kufanya biashara, kuongeza ushindani na uzalishaji wa biashara hizo. Serikali inaweza kufanya hivi kwa kuweka sera thabiti kwa kutegemea habari zinazofaa,” akasema Bw Karanja.

Janga la corona limesababisha biashara nyingi kufungwa na mamilioni ya Wakenya kupoteza ajira.Kulingana na Shirika la Takwimu Kenya (KNIBS), gharama ya maisha imekuwa ikiongezeka tangu janga hilo liliporipotiwa Kenya.

You can share this post!

Raia wafa njaa viongozi wakipiga domo

Umoja na KPA zashinda kwenye pambano la primia