• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wanafunzi wazimia shuleni kwa njaa

Wanafunzi wazimia shuleni kwa njaa

Na KENYA NEWS AGENCY

HOFU ilitanda katika Shule ya Msingi ya Kalimamundu, Kaunti Ndogo ya Kyuso, Kaunti ya Kitui, baada ya wanafunzi kadhaa kuzimia kutokana na makali ya njaa.

Mkurugenzi wa Elimu wa Kyuso, Stephen Mulandi, ameagiza usimamizi wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Kyuso kugawa chakula kwa wanafunzi wa shule ya Kalimamundu.

“Nimefahamishwa kuwa watoto walizimia kutokana na ukosefu wa chakula uliosababishwa na baa la njaa linaloshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi,” ikasema barua ya Bw Mulandi kwa mkuu wa shule ya Kyuso iliyoandikwa Agosti 24, 2021.

Bw Mulandi alisema ukosefu wa mvua kati ya Machi na Mei, mwaka huu 2021, umesababisha uhaba wa chakula katika eneo hilo.

Wakazi wa eneo hilo, wakiongozwa na Kathi Muthui, walichangisha chakula ili kuwasaidia watoto hao.

“Wengi wa waathiriwa wanatoka katika familia maskini,” akasema Bw Muthui.

Alisema kuwa wengi wa watoto wanaenda shuleni bila kula chochote kutokana na ukosefu wa chakula.

“Tunahitaji chakula zaidi kutoka kwa wahisani ili kusaidia shule hiyo na familia zisizokuwa na chakula,” akasema Kathi.

Alisema kuwa nzige waliovamia Kenya hivi majuzi, ukame na janga la corona vimechangia kwa baa la njaa katika eneo hilo.

Mnamo Aprili, serikali ilitangaza kuwa Wakenya milioni 1.4 walikuwa katika hatari ya kukosa chakula nchini.Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna alisema serikali ilikuwa mbioni kuhakikisha kwamba hakuna Mkenya ambaye anafariki kutokana na njaa.

Bw Oguna alisema kuwa uzalishaji wa chakula nchini ulidorora kutokana na uhaba wa mvua kati ya Oktoba na Desemba, mwaka 2020.

Wakenya kadhaa katika Kaunti ya Samburu wamefariki dunia kwa kukosa chakula na maji kufuatia ukame unaokumba kaunti 12 za eneo la Kaskazini Mashariki, Pwani na Mashariki mwa Kenya.

Athari za ukame pia zimeshuhudiwa kaunti za Turkana na Baringo eneo la Rift Valley ambako wakazi wanakodolea macho kifo kwa kukosa chakula na maji.

Vijiji kadhaa katika eneo la kaskazini mashariki vimejaa harufu ya mizoga ya mifugo wanaofariki kwa kukosa lishe na maji sawa na wenyeji wanaopaswa kuwatunza.

You can share this post!

Kianjokoma: Polisi mahabusu waomba DPP azimwe

Furaha mwanamume aliyetoweka miezi 8 iliyopita akirejea