• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Waislamu wakemea serikali kuhusu utekaji wa washukiwa wa ugaidi

Waislamu wakemea serikali kuhusu utekaji wa washukiwa wa ugaidi

WINNIE ATIENO na BRIAN OCHARO

VIONGOZI wa Kiislamu wameishutumu serikali kwa kuongezeka kwa visa vya kupotezwa kwa washukiwa wa ugaidi nchini.

Baraza Kuu la Waislamu nchini Kenya (Supkem), Muungano wa jamii ya Wasomali, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, Seneta Mohammed Faki badala yake wanaitaka serikali iwe ikiwapeleka kortini washukiwa.

Baadhi ya walioteweka kwa kutekwa nyara ni Abdulhakim Salim Sagar (Mombasa), Prof Abdiwahab Sheikh (Nairobi), Yassir Ahmed (Lamu), Alfani Juma (Mombasa) na Abdisatar Islam (Mombasa).

Wakizungumza mjini Mombasa, walisema kutoweka kwa mfanyibiashara Sagar kumeibua maswali mengi.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Bw Manase Mwania Musyoka alisema Bw Sagar, ambaye anahusishwa na ugaidi, hakukamatwa na kitengo chochote cha Huduma ya Polisi ya Kitaifa (NPS).

Katika sakabadhi za kortini, Bw Musyoka alikana kufahamu kuhusu kukamatwa kwa mshukiwa na maafisa wa polisi.

‘Hakuna wakati wowote Bw Sagar alikamatwa na au kuzuiliwa na polisi,’Lakini familia ya Sagar kupitia wakili Mbugua Murithi imeshutumu polisi kwa kushindwa kutoa maelezo ya mahali alipo mtu huyo.

“Maelezo ya gari hayapo katika mfumo wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA). Hili ni gari la nani ambalo NTSA haitaki kutoa maelezo yake? ” aliuliza wakili huyo.

Bw Sagar, 40, alitoweka mwezi uliopita akitokea Msikitini jioni wakati anadaiwa kukamatwa na watu wasiojulikana.

Kulingana na kakake Faris, watu takriban saba walimkabili Sagar na kumweka kwenye gari la Toyota Hilux lililokuwa likisubiri kabla ya kuondoka kwa kasi.

Familia yake inadai kuwa Bw Sagar alikuwa amepokea vitisho kabla ya kutekwa kwake.Sagar alikuwa na kesi ya ugaidi katika Korti ya Shanzu na amekuwa akiripoti kwa mpelelezi mara moja kwa mwezi.

You can share this post!

Wakazi wa Ol Moran wasita kurejea kwao

Uganda yaalika Rwanda uhusiano kati yao ukidorora