• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
ODM na PAA wazozania umiliki wa afisi mjini Malindi

ODM na PAA wazozania umiliki wa afisi mjini Malindi

Na MAUREEN ONGALA

MVUTANO umeibuka kuhusu umiliki afisi moja mjini Malindi kati ya chama cha ODM na chama kipya cha Pamoja African Alliance (PAA), chenye asili yake Pwani.

Vyama hivyo viwili vinavutana kuhusu ni chama kipi ambacho ni mkodishaji halisi wa afisi hiyo. Mvutano huo sasa umefikishwa mahakamani.

Ilidaiwa kuwa chama cha PAA kilitwaa afisi hiyo iliyoko katika jumba la Vera Cruiz mkabala na jumba la Malindi Complex lililoko kando ya barabara ya Lamu.

Afisi hiyo hutumika na Mshirikishi wa ODM kaunti ya Kilifi Justine Baya.Bw Justine alipata agizo la mahakama linalozuia Nairobi Homes, ambao ni maajenti wa mmiliki wa jengo hilo, Bw Naznin Mommed Shabir, kumfurusha kutoka afisi hiyo kwa kutolipa malimbikizi ya kodi ya Sh66,000.

Pia landilodi huyo alikuwa ametisha kupiga mnada mali ya afisa huyo wa ODM.Baada ya kupata agizo hilo la mahakama, Bw Baya alikodi vijana 30 wafuasi wa ODM kuchafua na kuweka kufuli katika afisi hiyo ambayo imetwaliwa na chama cha PAA.

Mnamo Septemba 10, Hakimu Mkuu wa Malindi William Chepseba alitoa agizo la kumzuia landilodi na maajenti wake au mtu yeyote kumfurusha Bw Baya.

Mahakama hiyo ilisema maajenti hao walikataa kuchukua kodi kutoka kwa mshirikishi huyo wa ODM.Kesi hiyo itasikizwa mnamo Septemba 21.

Akiongea na wanahabari katika afisi yake, Meneja wa Nairobi Homes, tawi la Malindi, Francis Mutungi alisema shida ilianza Baya aliposhindwa kulipa kodi kwa muda mrefu.

Alisema kufeli huko kulichangia wao kutafuta huduma za madalali ili waweze kupata pesa zao.Bw Mutungi alidai Bw Baya alikataa kulipa malimbikizi ya kodi hata baada ya kuagizwa na mahakama alipe.

“Tulipata agizo la mahakama ambalo lilituruhusu kupiga mnada mali ya Bw Baya. Baadaye tulipata mkodishaji mpya (chama cha PAA) ambaye alifuata utaratibu ufaao kupata afisi hiyo,” akasema.

Bw Mutungi alisema baada ya agizo hilo kutolewa, Bw Baya aliwasilisha malalamishi katika jopo la kusikitiza mizozo kati ya wapangaji na wenye nyumba.

Bw Baya alipata agizo la muda linalomruhusu kuendelea kukaa katika afisi hiyo.Lakini afueni hiyo kwa Bw Baya iliondolewa tena baada ya mawakili wa Nairobi Homes kuwasilisha ombi mahakamani.

“Madalali walitwaa mali kutoka kwa afisi ya Bw Baya, na afisi hiyo ikatangazwa kuwa wazi huku notisi ikiwekwa kuwaita wapangaji wapya,” Bw Mutungi akaongeza.

You can share this post!

Wilbaro, Chungwa vyazua mabishano

NYS sasa ni safi kama pamba, afisa mkuu asifia mageuzi