• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
CBC: Onyo wazazi wasifanyie watoto kazi za ziada

CBC: Onyo wazazi wasifanyie watoto kazi za ziada

Na FAITH NYAMAI

WAZAZI ambao watoto wao wanapata mafunzo chini ya mtaala mpya wa Umilisi na Utendaji (CBC) wametakiwa kukoma kuwasaidia watoto hao kufanya kazi za ziada wanazopewa na walimu wao.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) Charles Ong’ondo Ijumaa alisema badala yake alisema wazazi wanafaa kutoa kuhakikisha watoto wao wanapata vifaa vya kuwawezesha kufanya kazi hizo kivyao, bila kusaidiwa.

Hii ndio ya kuwawezesha watoto hao kupata uelewa na umilisi kulingana na mahitaji ya mtaala huo mpya. “Hakuna popote katika mtaala wa CBC ambapo wazazi wanahitajika kuwafanyia watoto wao kazi za ziada walizopewa na walimu wao. Kile wanahitajika tu kufanya ni kuhakikisha wanapata vifaa na mazingira bora ya kufanyia kazi hizo wao wenyewe,” akasema Profesa Ong’ondo.

Afisa huyo mkuu mtendaji alisema katika mwongozo kuhusu mtaala wa CBC, wazazi wako na jukumu la kuwasaidia tu watoto wao kufikia malengo ya mafunzo katika viwango mbalimbali.

Vile vile, wanahitaji kusaidia katika kufikiwa kwa malengo masomo kulingana na mwongozo wa walimu ili kuimarisha uelewa wa watoto.

Profesa Ong’ondo alitoa ufafanuzi huu baada ya baadhi ya wazazi kulalamika kwa watoto wao wanapewa kazi ngumu za ziada kufanyia nyumbani.

Wazazi hao pia wanadai mahitaji ya mtaala wa CBC ni ghali kwa sababu walimu haswa wale wa shule za kibinafsi wanawalazimisha watoto kununua vitabu na vifaa vingi vya masomo. Mnamo Alhamisi mzazi mmoja alielekea mahakama kutaka utekelezaji wa mtaala wa CBC usitishwe.

Kesi hiyo haijaratibiwa kusikizwa.Hata hivyo, kupitia wakili wake, Nelson Havi, mzazi huyo amemuomba Jaji Mkuu Martha Koome kuteua jopo la majaji watano kusikiza na kuamua kesi hiyo. Profesa Ong’ondo alisema mtaala huo anajumuisha masomo saba katika awamu na elimu ya msingi.

Walimu wanahitajika kukadiria uelewa na umilisi wa wanafunzi katika masomo hayo kupitia mijarabu ya kawaida na kazi za ziada wanazofanyia nyumbani.

Afisa huyo alisema mijarabu ya shuleni inalenga kuhakikisha kuwa watoto wanamilisi mbinu za mawasiliano, ushirikishi na wanaweza kuwa wabunifu ili wasuluhishe matatizo katika jamii.

“Vile vile, wanafunzi wataweza kupata masomo ya kidijitali, masomo ya uraia na mengine ambayo yanaweza kuwasaidia maishani,” Profesa Ong’ondo akaongeza.

You can share this post!

Raila tosha 2022, Joho asema

Tusker FC yaanza kunusia Sh60 milioni Klabu Bingwa Afrika...